Rais Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania imenufaika na misaada kutoka nchini Marekani kwa zaidi ya miaka sita ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa katika jitihada za taifa katika kuboresha maisha ya watanzania
Amesema hayo Machi 30, 2023 Ikulu jijini Dar es salaam wakati alipokutana na kuzungumza na Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris aliyefika nchini Machi 29, mwaka huu kwa ajili ya kuanza ziara yake ya siku tatu.
“Tunaishukuru Marekani kwa msaada katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, afya, chakula, demokrasia, haki za binadamu na utawala bora, kwa mfano katika UKIMWI na Kifua Kikuu havitishii tena maisha ya watu wetu,” amesema Rais Samia.
Wajue Marais wa Marekani waliowahi kuitembelea Tanzania kikazi
Aidha, Rais Samia amesema kupitia misaada ya Marekani, maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI yameshuka kutoka asilimia 7.2 mwaka 2012 hadi asilimia 4.7 mwaka 2016/2017 na kupungua zaidi mwaka 2021, huku vifo vya Malaria vikipungua kutoka milioni 7.7 mwaka 2015 hadi milioni 3.5, na kwamba jitihada zaidi zikifanyika Tanzania itapunguza zaidi vifo vitokanavyo na malaria.
Katika hotuba yake, Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris ametangaza kuwa Tanzania na Export-Import Bank ya Marekani zitatia saini makubaliano ambayo yatawezesha kufikia dola za Marekani milioni 500 (TZS trilioni 1.16) katika mauzo ya nje ya Marekani kwenda Tanzania, katika sekta za usafirishaji, miundombinu, teknolojia ya kidijitali na miradi ya nishati safi.
Pia, Marekani imeahidi kushirikiana na Tanzania katika teknolojia ya 5G, kupambana na uhalifu mtandaoni pamoja na kuwezesha uwekezaji mkubwa kutoka kwa wawekezaji wa Kimarekani katika sekta ya TEHAMA nchini.