Marekani yamwekea vikwazo Rais wa Zimbabwe na Makamu wa Rais kwa tuhuma za ufisadi

0
40

Marekani imemwekea vikwazo Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa na mkewe; Makamu wa Rais, Constantino Chiwenga; baadhi ya wakuu wa Serikali na mashirika matatu kwa madai ya ufisadi na ukiukaji wa haki za binadamu

Ofisi ya Idara ya Hazina ya Udhibiti wa Mali za Kigeni imesema viongozi nchini Zimbabwe wamekuwa wakipora rasilimali za umma kwa manufaa yao binafsi na kwamba kesi nyingi za utekaji nyara, unyanyasaji wa kimwili, na mauaji kinyume cha sheria zimewafanya wananchi kuishi kwa hofu.

“Shughuli hizi haramu zinasaidia na kuchangia mtandao wa uhalifu wa kimataifa wa hongo, magendo, na utakatishaji fedha unaosababisha umaskini kwa jamii nchini Zimbabwe, Kusini mwa Afrika, na sehemu nyingine za dunia,” imesema taarifa.

Vikwazo hivyo ni pamoja na kushikiliwa kwa mali zao zozote zilizopo kwenye ardhi ya Marekani na kutoruhusu safari zisizo rasmi nchini humo.

Rais Mnangagwa anatuhumiwa kuwalinda wasafirishaji wa dhahabu na almasi wanaofanya kazi nchini Zimbabwe na kuwaelekeza maafisa wa serikali kuwezesha uuzaji wa dhahabu na almasi katika masoko haramu, na kuchukua hongo ili kupata huduma zake.

Aidha, Marekani imesema vikwazo hivyo vya watu binafsi na mashirika haviathiri Zimbabwe wala raia wake.

Marekani kwa mara ya kwanza iliiwekea Zimbabwe vikwazo vya kiuchumi na vya usafiri mwanzoni mwa miaka ya 1990 ikimlenga Rais wa wakati huo, Robert Mugabe na makumi ya maafisa wengine wa ngazi za juu serikalini.

Send this to a friend