
Marekani inapanga kusitisha ufadhili wake kwa shirika la Utoaji wa Chanjo Duniani (GAVI) ikiwa ni sehemu ya juhudi za Rais Donald Trump kupunguza misaada ya kigeni.
Mkuu wa Gavi, Sania Nishtar, amesema shirika hilo bado halijapokea taarifa rasmi ya kusitishwa kwa ufadhili kutoka kwa serikali ya Marekani.
Hata hivyo, Gavi imesema inaendelea kuwasiliana na Ikulu ya Marekani na Bunge ili kuhakikisha wanapokea dola milioni 300 zilizotengwa kwa shughuli za mwaka 2025 pamoja na ufadhili wa muda mrefu.
Hata hivyo, Nishtar ametahadharisha kuwa kusitishwa kwa ufadhili kunaweza kutasababisha vifo vya zaidi ya watoto milioni moja kutokana na magonjwa yanayoweza kuzuilika kwa chanjo.
Wataalamu wa afya wamesema hatua hiyo itasababisha gharama kubwa kwa dunia kwa muda mrefu na inaweza kuharibu maendeleo yaliyopatikana katika miongo miwili na nusu ya kupambana na magonjwa hatari.