
Marekani imetangaza kufuta visa zote za watu wenye pasipoti ya Sudan Kusini baada ya nchi hiyo kushindwa kuwapokea raia wake waliorejeshwa kutoka Marekani kwa wakati unaofaa.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio amesema mbali na kufuta visa hizo, Marekani pia itazuia utoaji wa visa mpya kwa watu wa Sudan Kusini, ili kuwazuia kuingia nchini humo.
“Miadi yote ya visa imefutwa, hakuna visa mpya zitakazotolewa, na visa zilizopo hazitafanya kazi. Hakuna mtu yeyote kutoka Sudan Kusini atakayeingia Marekani hadi suala hili litakapopatiwa suluhisho,” imesema Wizara hiyo.
Taarifa ya Wizara imeongeza kuwa, “Tunalazimika kuchukua hatua hii kwa sababu kila nchi ina wajibu wa kuwapokea raia wake wanaporejeshwa kutoka nchi nyingine, ikiwa ni pamoja na Marekani.”
Aidha, Wazir Rubio, amesema Marekani iko tayari kutathmini upya hatua hizo iwapo Sudan Kusini itashirikiana kikamilifu.