Masauni: Tozo za miamala ya simu siyo jambo geni

0
69

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhandisi Hamad Yussuf Masauni amesema kodi ya miamala ya simu sio jambo geni nchini kwani huduma ya miamala kutoka Kampuni za Mawasiliano imekuwa ikitozwa fedha kwa anaetoa na anaepokea.

Masauni amesema hayo alipokuzungumza na Mabalozi wa Uhamasishaji wa Ulipaji Kodi kwa Hiari ambapo amewataka kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuelezea mafanikio ya Serikali yaliyopatikana kwa njia ya kulipa kodi ikiwa ni pamoja na miradi ya maendeleo.

Aidha, ametoa angalizo kwa baadhi ya kampuni simu kwa namna zinavyofanya promosheni yake kuhusu kodi ya Serikali kwa njia ya miamala kwa kutoa taswira mbaya pekee na sio faida zitakazo mgusa mwananchi moja kwa moja.

Ameeleza kuwa lengo la Serikali kuhusu kodi hiyo ni zuri ikiwa ni pamoja na kusaidia katika bima ya afya kwa wote, hivyo wale ambao hawana uwezo waweze kupata matibabu kwa uhakika na pia kushusha gharama za maisha kwa wananchi kwa kuweka miundombinu mizuri ya usafiri na usafirishaji itakayorahisisha maisha.

Hata hivyo amekumbusha kuwa tayari Rais Samia Suluhu Hassan alishatoa maelekezo kwa Waziri wa Fedha na Mipango kuhusu kuunda timu ya wataalamu ili waweze kuona ni namna bora ya kuboresha kodi hiyo ikiwa ni pamoja na kuangalia marekebisho ya sheria.

Mhandisi Masauni amewapongeza mabalozi wa kuhamasisha kulipa kodi kwa hiari kwa kuonesha nia ya dhati katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi na kujua umuhimu wa kulipa kodi kwa maendeleo yao.

Kwa upande wao mabalozi, wameipongeza Serikali kwa hatua yake ya kuwateua na kutambua umuhimu wao katika uhamasishaji, na wameahidi kufanya kazi kwa bidii katika jukumu hilo.

Send this to a friend