Maswali na majibu kuhusu ugonjwa wa Corona (Covid19)

0
46

Imeandikwa na Dr Norman Jonas kupitia mtandao wa Medium.

Kwa msaada wa machapisho rasmi ya shirika la afya duniani — WHO

Dhumuni ni kusaidia wazungumzaji wa kiswahili kupata taarifa sahihi Ugonjwa wa Corona COVID19.

01. VIRUSI VYA CORONA NI NINI?
Virusi vya Corona ni familia kubwa ya virusi ambayo huweza kusababisha maradhi kwa binadamu na wanyama. Kwa binadamu; kuna aina kadhaa za virusi vya corona ambazo husababisha maambukizi ya njia ya hewa kuanzia mafua ya kawaida hadi magonjwa makali kama Ugonjwa wa corona wa MERS , SARS na sasa ugonjwa wa corona COVID-19.

02. UGONJWA WA CORONA COVID19 NI NINI?

Huu ni ugonjwa wa kuambukiza ambao umesababishwa na kirusi aina mpya cha corona. Aina hii ya kirusi na ugonjwa ulikuwa haujulikani ni mpya, ulianzia jiji la Wuhan, China mwezi Disemba 2019.

03. DALILI ZA UGONJWA WA CORONA COVID19 NI ZIPI?

Dalili za ugonjwa wa Corona COVID19 kwa wagonjwa wengi ni homa, uchovu na kikohozi kikavu. Wagonjwa wengine hupata dalili kama misuli kuuma, pua kubana, mafua kutiririka, maumivu ya koo au kuharisha. Dalili hizi huwa ni ndogo na huanza taratibu. Baadhi ya watu huambukizwa na hawapati dalili yoyote. Katika wagonjwa 100 wa ugonjwa wa Corona wagonjwa 80 hupona ugonjwa wenyewe bila kuhitaji matibabu mkubwa. Ni mgonjwa mmoja kati ya 6 aliyeambukizwa virusi wa Corona COVID19 hupata ugonjwa mkubwa na kupata shida ya kupumua. Wazee, watu wenye shida nyingine za afya kama shinikizo kubwa la damu, matatizo ya moyo au kisukari huwa na uwezekano wa kupata dalili mbaya. Ni asilimia 2 tu ya watu walioambukzwa virusi vya Corona COVID19 wamefariki. Watu walio na dalili kama homa, kikohozi na shida ya kupumua watafute msaada wa kitiba.

04. JE UGONJWA WA CORONA COVID19 UNASAMBAA VIPI?

Ugonjwa wa corona husambaa kutoka kwa mtu hadi mtu kupitia vitone vidogo vidogo vya mate vinavyoruka toka puani au mdomoni bali mtu mwenye maambukizi ya virusi vya Corona COVID19 anapopiga chafya , kukohoa au kupumua. Vitone hivi vya mate huweza kutua kwenye nyuso za vitu hivyo watu wengine hupata virusi hivi wanapogusa hivi vitu. Vitone hivi vikiruka hewani mtu anapopiga chafya au kukohoa mtu mwingine huweza kuvivuta ndani na hewa anapopumua hivyo huwa ni muhimu kukaa umbali wa mita 1 kutoka kwa mtu anayeumwa

05. JE UNAWEZA VIPI KUJIKINGA NA MAAMBUKIZI YA UGONJWA WA CORONA COVID19

Jambo muhimu kuliko yote ni kufuatilia taarifa sahihi kuhusu mlipuko wa ugonjwa wa Corona unavyoendelea. Fuatilia kupitia vyombo sahihi kama shirika la afya duniani, wizara ya afya na vyombo rasmi vya afya ya jamii. Watu wengi wanaopata maambukizi ya virusi vya corona hupata dalili za wastani na kupona lakini dalili huweza kuwa mbaya kwa baadhi.
Linda afya yako na wengine kwa kufanya yafuatayo:

  1. Nawa mikono mara kwa mara kwa maji na sabuni au kutumia dawa maalumu ya kuua wadudu (Hand sanitizer)
    Kwa nini? Ukinawa mikono kwa sabuni na maji au kutumia dawa maalumu ya kusafisha mikono utaua virusi ambao hukaa kwenye mikono mara nyingi
  2. Jiweke mbali zaidi ya mita moja kutoka kwa mtu anayekohoa au kupiga chafya.
    Kwa nini? Mtu anapopiga chafya au kukohoa hurusha chembechembe za mate ambazo huweza kuwa zimebeba virusi. Ukiwa karibu sana utawavuta virusi hawa unapovuta hewa kupumua.
  3. Acha kushikashika macho, pua na mdomo kwa mikono ambayo hujaisafisha
    Kwa nini? Mikono hugusa sehemu mbalimbali hivyo huweza kubeba virusi. Unapogusa macho ,pua au mdomo virusi hupata njia ya kuingia mwilini na kukufanya uugue.
  4. Iwapo unaumwa mafua, homa au shida ya kupumua usiendelee na shughuri zako nenda hospitali
    Kwa nini? Vituo vya huduma ya afya vina taaarifa zote kuhusu mlipuko wa ugonjwa wa corona pia huweza kukupatia tiba sahihi kuhusu tatizo lako pia hukulinda na kusaidia usisambaze maambukizi kwa watu wengine.

06. NI KWA URAHISI GANI NAWEZA KUAMBUKIZWA UGONJWA WA CORONA COVID19?
Uwezekano wa mtu kuambukizwa virusi vya Corona hutegemea unaishi eneo gani na iwapo umesafiri karibuni. Uwezekano wa maambukizi ya Corona COVID ni kwenye maeneo ambayo yana mlipuko tayari wa Ugonjwa wa Corona hasa China na maeneo ya bara la Asia. Maeneo mengine uwezekano ni mdogo ni muhimu kufuatilia taarifa rasmi kutoka vyombo rasmi.

07. JE UNATAKIWA KUWA NA HOFU KUBWA KUHUSU KUAMBUKIZWA UGONJWA WA CORONA?
Kama hauishi katika maeneo ambayo ugonjwa wa corona COVID19 umesambaa au hujawahi kusafiri nje ya nchi kwenye maeneo yenye mlipuko au kuwa karibu na mtu anayeshukiwa kuwa na ugonjwa wa Corona uwezekano wako wa kupata maambukizi ya ugonjwa wa Corona ni mdogo sana. Hutakiwi kupaniki na kushindwa kufanya shughuri zako.
Ni muhimu kufuatilia taarifa sahihi kutoka vyombo vya wizara ya afya, mwajiri wako au wataalamu wa afya wa eneo lako.

08. JE NI NANI HUPATA DALILI MBAYA ZA UGONJWA WA CORONA COVID19?

Bado wanasayansi na watafiti wanajifunza namna ugonjwa wa Corona COVID19 unavyoathiri watu. Lakini uchunguzi wa awali unaonyesha dalili mbaya za ugonjwa wa corona hupata zaidi wazee na watu wenye magonjwa ya kudumu kama kisukari, shinikizo kubwa la damu, magonjwa ya moyo.

09. JE KUNA CHANJO AU DAWA YA KUTIBU UGONJWA WA CORONA?

Mpaka wakati huu hamna chanjo wala dawa maalumu ya kutibu ugonjwa wa corona COVID19. Lakini wagonjwa wa Corona hupatiwa matibabu kutibu dalili za ugonjwa. Matibabu haya husaidia wagonjwa wengi kupona. Shirika la afya duniani linafanya kazi kuratibu tafiti za chanjo na tiba ya ugonjwa wa Corona.

10. JE KUNA ULAZIMA WA KUVAA MASK ILI NISIAMBUKIZWE UGONJWA WA CORONA?

Shirika la afya duniani linashauri matumizi ya mask kwa wafanyakzi wa afya na watu wanaohudumia wagonjwa nyumbani. Kwenye maeneo yasiyo na mlipuko wa ugonjwa wa corona haina haja ya kuvaa mask. Watu wenye ugonjwa wa mafua, kikohozi huitaji kuvaa mask ili kuepuka kusambaza maambukizi.

11.JE DALILI ZA UGONJWA WA CORONA HUANZA KUONEKANA MUDA GANI BAADA YA KUAMBUKIZWA?

Inakadiriwa wagonjwa wa Corona COVID19 huanza kunyesha dalili za ugonjwa wa corona siku 1 hadi 14 baada ya maambukizi. Kwa wastani dalili hutokea siku ya 5

12. JE NAWEZA KUAMBUKIZWA UGONJWA WA CORONA KUTOKA KWA WANYAMA?

Chanzo halisi cha ugonjwa wa corona COVID19 bado hakijathibitishwa tafiti zinaendelea kutafuta chanzo cha Corona.

13. JE VIRUSI VYA CORONA VINAWEZA ISHI KWENYE MAZINGIRA NA NYUSO ZA VITU KWA MUDA GANI?

Tafiti za awali zinaanza kuonyesha kuwa virusi vya Corona COVID19 huweza kuishi kwenye nyuso za vitu na mazingira kwa masaa kadhaa hadi siku. Utofauti wa muda hutegemea na hali tofauti za kimazingira kama aina ya kitu, halijoto ya mahali au unyevunyevu.

Iwapo unahisi vitu flani vimegusa virusi vya Corona, unaweza takasa kutumia vitakasaji kama dettol. Nawa mikono kwa maji na sabuni

14.JE NAWEZA AMBUKIZWA UGONJWA WA CORONA KUPITIA KUPOKEA MIZIGO KUTOKA NJE?

Uwezekano kupata virusi vya Corona kupitia mizigo ni kidogo sana kwa sababu mizigo hupitia katika hali mbalimbali na joto hivyo virusi hufariki baada ya muda mfupi.

15. MAMBO GANI SIRUHUSIWI KUFANYA KUHUSIANA NA UGONJWA WA CORONA COVID19?

Epuka kuamini uvumi wa kuhusu matibabu, njia sahihi za matibabu na namna ya kujikinga zinatolewa na shirika la afya duniani na wizara ya afya. Njia nyingi za matibabu zinazotolewa kupitia uvumi huweza kuwa na madhara.

Njia hizi hazina ufanisi katika kutibu ugonjwa wa Corona COVID19 :

  • Sigara
  • Dawa za kienyeji ambazo hazijathibitishwa na shirika la afya duniani au wizara ya afya
  • Iwapo una homa, kikohozi na shida ya kupumua, Tafuta msaada wa kiafya mapema ili kupunguza hatari ya kupata dalili mbaya. Hakikisha umemwambia mtoa huduma kuhusu historia yako ya kusafiri.

MUHIMU

Fuatilia taarifa kuhusu ugonjwa wa Corona COVID19 kupitia vyombo sahihi vya taarifa vya Shirika la afya duniani na wizara ya Afya.

  1. Tovuti maalum ya shirika la afya duniani ya taarifa za kila siku kuhusu mlipuko wa ugonjwa wa corona COVID19 https://www.who.int/emergencies/diseases/novel-coronavirus-2019/events-as-they-happen
  2. Tovuti inayotoa taarifa za moja kwa moja kuhusu ugonjwa wa Corona COVID19 https://experience.arcgis.com/experience/685d0ace521648f8a5beeeee1b9125cd

Asante

Na : Dr Norman Jonas

Send this to a friend