
Rais Donald Trump Jumatano ametangaza kuwa Marekani itaweka ushuru wa asilimia 10 kwa kila nchi duniani, huku viwango vya juu zaidi vikilenga washirika wake wakuu wa kibiashara, ikiwa ni pamoja na China, India, Japan, Korea Kusini, Uingereza, na Umoja wa Ulaya. Habari hiyo ilisababisha kuporomoka kwa masoko ya hisa duniani.
Kuporomoka huko kumesababisha hasara ya pamoja ya dola bilioni 270 kutoka kwa matajiri 3,000 duniani. Walioathirika zaidi ni matajiri wakubwa, hasa wale walioonekana kuwa karibu na Trump katika siku za hivi karibuni.
Mtu aliyepata hasara kubwa zaidi ni mwanzilishi wa Meta, Mark Zuckerberg, ambaye amepoteza dola bilioni 17.9 tangu kufungwa kwa soko la hisa jana, baada ya hisa za Meta kushuka kwa asilimia 9. Zuckerberg, aliketi karibu na Jeff Bezos na Elon Musk wakati wa kuapishwa kwa Trump mwezi Januari, na kampuni yake ilichangia katika kamati ya uapisho wa Trump, pia amekutana na Rais mara kadhaa katika Ikulu ya Marekani, mara ya mwisho ikiwa Jumatano.
Mwingine aliyepata pigo kubwa ni Jeff Bezos wa Amazon, ambaye hivi karibuni amekuwa akijaribu kuwa karibu na Trump. Bezos, aliyeketi nyuma ya rais wakati wa uapisho wake Januari, pia alitangaza Februari kwamba gazeti lake, The Washington Post, lingebadilisha safu yake ya maoni ili kuzingatia uhuru wa mtu binafsi na masoko huria.
Mwezi mmoja baadaye, alizungumzia ushuru huo katika chapisho la X, akisema kuwa “ushuru wa forodha unaweza kuleta madhara katika uchumi.” Kwa kushuka kwa hisa za Amazon kwa asilimia 9, Bezos sasa amepoteza dola bilioni 16.
Larry Ellison, mwanzilishi wa Oracle, alipoteza dola bilioni 9.9 baada ya hisa za kampuni yake kushuka kwa asilimia 6. Tofauti na Bezos na Zuckerberg, Ellison amekuwa mfadhili wa muda mrefu wa chama cha Republican na aliandaa harambee ya kuchangia kampeni ya Trump mwaka 2020. Mwezi Januari, alijiunga na Rais kutangaza uwekezaji wa dola bilioni 500 kwenye vituo vya data vya AI nchini Marekani.
Elon Musk, mtu tajiri zaidi duniani na mshirika wa karibu wa Trump katika Idara ya Ufanisi wa Serikali, pia amepata hasara kubwa. Musk amepoteza dola bilioni 8.7, huku hisa za Tesla zikiporomoka kwa zaidi ya asilimia 5 baada ya kampuni hiyo kutangaza kushuka kwa mauzo kwa asilimia 13 katika robo ya kwanza ya mwaka huu.
Hata hivyo, kwa Trump, hali si mbaya sana. Utajiri wake umepungua kwa dola milioni 40, kufikia dola bilioni 4.6, huku kampuni yake Trump Media & Technology Group Corp. ikishuhudia kushuka kwa hisa kwa 3%, kiwango kidogo ukilinganisha na mporomoko wa soko lote.
Orodha ya matajiri 10 walioathirika zaidi na ushuru mpya wa Trump (TZS);
1. Mark Zuckerberg
Chanzo cha utajiri: Facebook
Utajiri wa jumla: Trilioni 490.6
Hasara: Trilioni 47.7
2. Jeff Bezos
Chanzo cha utajiri: Amazon
Utajiri wa jumla: Trilioni 522.9
Hasara: Trilioni 42.6
3. Larry Ellison
Chanzo cha utajiri: Oracle
Utajiri wa jumla: Trilioni 459.7
Hasara: Trilioni 26.4
4. Michael Dell
Chanzo cha utajiri: Dell Technologies
Utajiri wa jumla: Trilioni 226.2
Hasara: Trilioni 25
5. Elon Musk
Chanzo cha utajiri: Tesla, SpaceX
Utajiri wa jumla: TZS quadrilioni 1
Hasara: Trilioni 23.1
6. Bernard Arnault
Chanzo cha utajiri: LVMH
Utajiri wa jumla: Trilioni 409.2
Hasara: Trilioni 22.8
7. Jensen Huang
Chanzo cha utajiri: Sekta ya semiconductor
Utajiri wa jumla: Trilioni 237.3
Hasara: Trilioni 19.7
8. Larry Page
Chanzo cha utajiri: Google
Utajiri wa jumla: Trilioni 335.8
Hasara: Trilioni 13
9. Sergey Brin
Chanzo cha utajiri: Google
Utajiri wa jumla: Trilioni 322
Hasara: Trilioni 12.2
10. Thomas Peterffy
Chanzo cha utajiri: Uwakala wa udalali wa hisa (Discount brokerage)
Utajiri wa jumla: Trilioni 128.6
Hasara: Trilioni 10.9
Chanzo: Forbes