Matajiri kununua uraia wa Marekani kwa bilioni 12

Rais Donald Trump ametangaza mpango mpya wa kuuza “kadi za dhahabu” kwa dola milioni 5 [TZS bilioni 12.9], ambao utawapa wageni matajiri haki ya kuishi, kufanya kazi nchini humo, na hatimaye kupata uraia wa Marekani.
Trump amesema mpango huo utachukua nafasi ya mpango wa zamani wa EB-5, ambao uliwaruhusu wawekezaji wa kigeni kupata ‘green card’ kwa kuwekeza katika miradi inayozalisha ajira nchini Marekani.
“Mnaijua kadi ya kijani (green card), hii ni kadi ya dhahabu. Tutaiuza kwa takriban dola milioni 5, na hiyo itawapa wahusika haki sawa na wenye kadi ya kijani, pamoja na njia ya kupata uraia. Watu matajiri wataweza kuingia nchini mwetu kwa kununua kadi hii,” amesema kutoka Ikulu ya Marekani.
Alipoulizwa na mwandishi wa habari ikiwa marafiki zake matajiri kutoka Urusi wataweza kupata kadi hiyo, Trump amejibu: “Ndio, huenda ikawa hivyo. Nawajua baadhi ya matajiri wa Urusi ambao ni watu wazuri sana.”
Trump amesema mpango huo unatarajiwa kuanza rasmi ndani ya wiki mbili zijazo.