Matokeo ya utafiti ugonjwa wa kizunguzungu kwa mbuzi na kondoo

0
90

Mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Dk. Jahashi Nzalawahe ametoa taarifa ya matokeo ya utafiti wa ugonjwa wa kizunguzungu cha mbuzi na kondoo katika halmashauri ya Wilaya ya Babati mkoani Manya.

Dk. Nzalawahe amebainisha kuwa kwa kiasi kikubwa ugonjwa huo huchangiwa na minyoo tegu ambayo hupatikana kwenye kinyesi cha mbwa na kwamba anapojisaidia kuna pingili za mayai zinapasuka na kuacha mayai kwenye majani.

Ummy: Hakuna mgonjwa mpya Homa ya Mgunda

Aidha, Dk. Nzalawahe amesema baadhi ya dalili za ugonjwa huo ni kuzubaa kwa mnyama, kuanza kujitenga na wenzake, kupooza shingo, miguu, mgongo, kuzimia, macho kupofuka na kutafuna meno, na mwishowe mnyama hufariki.

Nao baadhi ya wafugaji wilayani Babati, akiwemo Dorcas Bayai kutoka kijiji cha Minjigu, Kata ya Ngaiti amesema kwa muda mrefu Kata yao imekuwa ikisumbuliwa na ugonjwa huo bila kujua unatokana na nini.

Ameongeza kuwa wafugaji wanapokuwa wakiona mbuzi au kondoo ana dalili za ugonjwa huo humchinja, mara nyingi kwenye kichwa hukuta uvimbe na wadudu kisha hutoa eneo hilo na kulitupa.

Taarifa ya Dk. Nzalawahe inasema tiba ya ugonjwa huo bado haijapatikana, hivyo watafiti wa magonjwa ya mifugo (SUA) wameomba ufadhili wa Serikali kupitia Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) ili kudhibiti maambukizi.