Matokeo ya majaribio ya dawa ya dexamethasone yaliyofanyika nchini Uingereza yameonesha kuwa inaweza kuokoa maisha ya watu walio mahututi wanaougua ugonjwa wa homa ya mapafu (Covid-19).
Shirika la Afya Duniani (WHO) limefurahishwa na matokeo dawa hiyo ambapo kwa wagonjwa wanaotumia mashine za kupumua, dawa hiyo imepunguza idadi ya vifo kwa theluthi moja, na kwa wagonjwa wanaohitaji hewa ya oksijeni, idadi ya vifo imepungua kwa moja ya tano.
“Hii ndio dawa ya kwanza kupunguza idadi ya vifo kwa wagonjwa wa virusi vya corona wanaohitaji oksijeni au walio kwenye mashine za kupumua,” amesema Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus.
Dexamethasone ni dawa ambayo imekuwa ikitumiwa tangu 1960 kupunguza uvimbe katika hali tofauti kama vile ugonjwa wa saratani na yabisi kavu.
Dawa hiyo ni miongoni dawa nyingi zinazoendelea kufanyiwa majaribio duniani kote ili kupata dawa itakayoweza kukabiliana na virusi vya corona.
Watafiti wanakadiria kwamba iwapo dawa hiyo ingekuwepo nchini Uingereza kuanzia mwanzo wa mlipuko wa corona , hadi maisha ya watu 5000 yangekuwa yameokolewa.