Kocha Msaidizi wa Simba, Seleman Matola amethibitishia kuondoka kwenye benchi la ufundi la timu hiyo kwa muda akieleza kuwa anakwenda kuongeza elimu yake.
Nahodha huyo wa zamani wa Simba na Taifa Stars, amepata fursa ya kwenda kusoma kozi ya leseni A ya CAF na ataanza Novemba 21 ambapo atasoma kwa wiki mbili, kisha atarejea kikosini hapo kwa ajili ya kufanyia kazi kwa vitendo mafunzo aliyoyapata.
“Nisingeweza kukataa fursa hiyo, lakini sitaacha kuitakia mema timu yangu, nitakuwa nawasiliana na kocha, kuhakikisha tunashauriana ili Simba ibaki kuwa imara kwa muda wote inapocheza ligi ya ndani na Ligi ya Mabingwa Afrika.
Nilishaongea na viongozi kila kitu kuhusu kozi hii, naamini watakuwa wanalifanyia kazi suala hilo, Simba ni klabu kubwa itaweka sawa kila kitu, zaidi ya hayo yote namshukuru Mungu kupata fursa hiyo na uzuri nitakuwa narejea kwenye klabu yangu kufanya mafunzo ya vitendo.” amesema.