Matukio makubwa katika safari ya ukocha ya Didier Gomes Da Rosa
Simba SC leo imevunja mkataba na kocha wake Didier Gomes Da Rosa, ikiwa ni miezi 9 tangu kupewa kibarua hicho cha kuwanao miamba hao wa Kariakoo, Dar es Salaam.
Gomes alizaliwa Oktoba 10, 1969 huko Charenton-le-pont nchini Ufaransa. Amepata mafaniko mbalimbali katika soka, ambayo ni pamoja na:
Mwaka 2013 alitwaa taji la Ligi Kuu nchini Rwanda akiwa na klabu ya Rayon Sports.
Mwaka 2014 na 2015 alitwaa taji la ligi ya Cameroon akiwa na klabu ya Cotton Sports FC.
Baada ya kufanya vizuri nchini Rwanda, mabosi wa Rayon Sports walitaka kumuongeza mkataba, jambo ambalo yeye alilikataa kwa kuwa alihisi ameshakamilisha huduma yake nchini humo.
Gomes akajiunga na CS Constantine ya nchini Algeria kwa kandarasi ya miaka miwili na kuiokoa timu hiyo kushuka daraja kwa kuwa ilikuwa na hali mbaya.
Mwezi Machi 2019 alijiunga na Horoya AC ya nchini Guinea ambapo hakudumu, alifukuzwa mwezi Novemba kwa sababu za kiufundi na kwa kupoteza mechi 3 kwenye mechi 6 alizocheza na kushinda mbili huku akitoa sare mechi moja.
Januari 2020 Ismaily SC ilimtangaza Didier Gomes kama kocha wao mpya. Aliiwezesha timu hiyo kufika nusu fainali ya Arab Cup.
Disemba 14, 2020 kocha huyo alijiunga na Al Merrikh ya Sudan na kuiwezesha kufuzu katika hatua ya makundi, hatua ambayo timu hiyo ilikuwa haijafikia kwa miaka kadhaa.
Gomes alitua Simba Januari mwaka huu akichukua mikoba ya Sven van Derbroek kunako viunga vya msimbazi.
Akiwa na Simba ameweza kutwaa mataji matatu ya Ligi Kuu Tanzania Bara, Kombe la Shirikisho na Simba Super Cup.