Mawasiliano ya barabara katika Daraja la Somanga yarejea

0
41

Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imesema mawasiliano ya barabara kuu ya kutoka Dar es Salaam na mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara yarejea katika eneo la Somangafungu mkoani Lindi kutokana na daraja la Somanga linalounganisha barabara hiyo kukatika na kusababisha barabara hiyo kufungwa kwa saa kadhaa.

Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Lindi, Eng. Emil Nzengo amesema tayari magari ya abiria na mizigo na vyombo vingine vya usafiri vimeruhusiwa kupita upande mmoja katika daraja hilo ambalo lilikuwa halipitiki tangu usiku wa kuamkia leo kutokana na mvua zinaoendelea kunyesha mkoani humo.

“Tumekamilisha kazi awamu ya kwanza, wananchi na magari wameruhusiwa kuanza kupita. Tunawashukuru wananchi kwa uvumilivu na tunaomba waendelee kuiamini Serikali ipo kazini kwa ajlili yao,” amesema Eng. Nzengo.

Awali, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa alieleza kuwa jitihada kubwa zinaendelea za kurudisha mawasiliano ya barabara eneo la Somangafungu na kuagiza timu ya Wataalam kutoka TANROADS kuhakikisha hadi kufikia Machi 25, 2024 mawasiliano yawe yamerejeshwa na magari yaanze kupita katika daraja hilo.

Send this to a friend