Watu 14 wamefikishwakatika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani Mbeya na kufunguliwa kesi ya Uhujumu Uchumi Namba 03/2023 wakituhumiwa kuendesha genge la uhalifu kinyume Sheria ya Uhujumu Uchumi.
Washitakiwa wanatuhumiwa kutenda kosa hilo kwa kutengeneza mfumo haramu wa kukusanya ushuru wa mazao wilaya za Mbarali, Rungwe, Mbeya, Ileje na Momba na kufanikiwa kukusanya TZS milioni 382.8.
Pamoja na shitaka hilo, mshitakiwa wa nne hadi mshitakiwa wa 14 wameshitakiwa pia kwa kosa la kumiliki kifaa haramu kinyume na kifungu cha 10(1)(a) cha Sheria ya Makosa ya Mtandao. Washitakiwa hao wameshitakiwa kwa kosa hilo baada ya kukutwa wakimiliki mashine za POS ambazo zilikuwa na mfumo haramu wa kukusanyia ushuru wa mazao.
Aidha, mshitakiwa wa kwanza, tatu na 14 wameshitakiwa kwa makosa ya utakatishaji fedha kinyume na kifungu cha 12(b) na 13(1)(a) cha Sheria ya Utakatishaji Fedha. Wanatuhumiwa kutumia fedha walizozipata kutokana na kukusanya ushuru wa mazao kwa njia harumu kununulia viwanja na nyumba ili kuficha ukweli juu ya uchafu wa pesa husika.
Baada ya kusomewa mashitaka hayo hawakupaswa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo bado haijapewa mamlaka ya kusikiliza shauri.
Washitakiwa wote wamerejeshwa rumande kwa kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi haina mamlaka ya kutoa dhamana kwa shauri la jinai ambalo kiasi cha fedha inayotuhumiwa ni zaidi ya TZS milioni 300.
Kesi hiyo itatajwa Septemba 11 mwaka huu.