Mbinu za kisayansi zilizotumika kusambaza mabango ya Imani, Upendo na Miujiza

0
81

Ni wazi kuwa kwa asilimia kubwa ya wakazi wa Dar es Salaam ama wameona mitaani au kwenye mitandao ya kijamii namna mabango ya mkutano wa injili yalivyotapakaa kuanzia kwenye nguzo za umeme, kuta za madaraja, viwanja vya michezo, vituo vya daladala na daladala zenye mkoani humo.

Cha ajabu zaidi, baadhi ya wananchi hao wamesikika wakisema kuwa huwa hawaoni watu wakibandika, lakini wakiamka asubuhi wanakuta tayari mji unang’aa rangi ya njano, na macho yao yanashindwa kukwepa kusoma mabango hayo yenye ujumbe ulioshika kasi wa ‘Imani, Upendo, Miujiza.’

Hii si mara ya kwanza kwa huduma ya Christ for All Nation (CFAN) kufika Tanzania, lakini kitendo cha kubandika mabango kwa ukubwa huu, hakijawahi kufikiwa, hali iliyosababisha wao kuwa gumzo mtaani.

Mmiliki wa kampuni hiyo ambayo inafanya kazi na CFAN ameeleza kuwa usambazaji wa mabango hayo haukufanyika ilimradi, bali umefanyika kisayansi na kwamba walikuja na mpango mkakati wa namna ya kusambaza mabango hayo kuhakikisha kuwa kila mtu anaona, na asiwe na uwezo wa kukwepa kutokuyaona.

Amesema wakati wanakuja tayari walikuwa na kila kitu walichotaka na namna walivyotaka kufanyike, na kwamba wao (yeye na timu yake) jukumu lao ilikuwa ni kusambaza tu. Ameongeza kuwa wao (CFAN) walikuwa wanajua taarifa muhimu kama wapi pana watu wengi, njia ipi inapita magari mengine, maeneo ya wazi, maeneo yenye nguzo za umeme hivyo alishajua ni wapi wataweka mabango na wataweka kwa idadi gani.

Ameeleza zaidi kwamba wingi wa mabango hayo ulifanya makusudi kuhakikisha wananchi hawawezi kukwepa kuyaona, na pia yaliwekwa mengi ili mtu akichana moja au mawili, bado yabaki mengine yatakayoonesha ujumbe.

Waandaaji hao walituma watu kuja nchini kabla ya usambazaji haujaanza, na walizunguka maeneo mbalimbali kwa kutumia ramani na kukusanya taarifa muhimu ambazo ziliwezesha usambazaji wa mabango hayo kuwa madhubuti kama ilivyodhirika.

“Wewe unaweza kukadiria sehemu fulani kuwa watu 200, lakini yeye anakwambia ‘hapana, kuna watu 4000,” amesema mmiliki huyo. Ameongeza kwamba walikuwa na taarifa nyingi mfano ni muda gani barabara mfano, Ubungo-Mbezi inakuwa na magari mengi, na muda gani yanapungua, hivyo wanajua ni wapi pakuweka mabango mengi.

Ameongeza kuwa tangu mwaka 2020 kuna watu walikuwa wanamuuliza gharama za kuweka mabango, kumbe kwa kufanya vile walikuwa wanakusanya taarifa mapema, hivyo ikifika wakati wa kutekeleza jukumu lao, wanakuwa na taarifa zote za msingi.

Licha ya kazi hiyo kubwa, baadhi ya watu wameeleza kutofurahishwa kwao na mabango hayo, huku wakitaka mamlaka husika kuwachukulia hatua wote waliosambaza kwa maelezo kwamba wamechafua mji.

Kwa upande mwingine baadhi ya watu wametaka mamlaka kuhakikisha kwamba baada ya mkutano huo, mabango yote yanaondolewa.