Mbowe: CHADEMA hakitakuwa chama kikuu cha upinzani milele

0
22

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) amesema kuwa chama hicho hakitakuwa chama kikuu cha upinzani milele, na hivyo amekiasa kushirikiana na vyama vingine vya upinzani, ili hata kitakapoondoka uhusiano wao mzuri uendelea.

Mbowe amesema hayo leo akizungumza katika Baraza Kuu la CHADEMA mkoani Dar es Salaam ambapo ametumia jukwaa hilo kuwaonya viongozi na wanachama wa chama hicho kutokuwatusi wanachama wa vyama vingine pindi wanapotofautiana kimtazamo.

“…yawezekana kesho ikawa ni ACT, yawezekana keshokutwa ikawa ni Mzee Rungwe, yawezekana ikawa ni CUF, ama chama chochote kile. Kwa hiyo wakati wote, chama chetu kinapaswa kuwa wanyenyekevu kwa vyama vingine vya siasa, kwa maamuzi ya vyama vingine vya siasa, tuheshimu mitazamo ya vyama vingine vya siasa,” ameelekeza.

Aidha, amesema CHADEMA “kifanye kazi ya kujenga harakati za kweli na sio kazi ya kutukana vyama vingine aidha kwenye
mitandao, kwenye mikutano au mahali popote.”

Ameongeza kuwa anaona kwenye mitandao maneno ya bughudha, maneno ya maudhi ambayo viongozi wa CHADEMA wanafanya kudhalilisha vyama vingine, na hivyo ameagiza vitendo hivyo kukoma mara moja.

“Tuheshimu vyama vya wenzetu, tuheshimu mawazo yao. Tunapotofautiana ndio demokrasia yenyewe,” amesisitiza, huku
akiwasihi wanachama wa chama hicho kutumia nguvu kujenga CHADEMA itakayolisaidia.