Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe amesema amepoteza mabilioni ya fedha kwa kuwa mwanachama wa CHADEMA na kukitumikia chama hicho kwa kushiriki katika harakati za kupigania haki za Watanzania.
Akizungumza leo Januari 21, 2023 katika ufunguzi wa mikutano ya hadhara ya chama hicho uliofanyika jijini Mwanza, Mbowe ameyasema hayo kufuatia kauli ya wanachama na baadhi ya viongozi kudai kuwa amepewa rushwa na Serikali ili kwenda kinyume na misimamo ya chama hicho.
“Napenda kuwaambia Wana-CHADEMA, jambo hili liliniumiza siyo mimi, watoto wangu, wanangu, mke wangu kwa sababu wanajua Mbowe nimepoteza mabilioni mangapi kwenye kuitetea haki na demokrasia ya nchi yangu. Anatoka kiongozi anasema Mbowe nimekula asali na anataka kuiaminisha umma Kwamba Mbowe mimi nimekula asali,” ameeleza.
Aidha, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Abdulrahman Kinana na kuweka wazi kuwa hatoacha kutambua ustahimilivu wao ambao walipambana na kupata upinzani mkubwa ndani ya chama chao lakini waliridhia kuweka vyama pembeni na kusimama katika misingi ya kujenga nchi.
“Wakati viongozi wenzangu na wanachama ndani ya chama changu wanalalamika, hata ndani ya chama chao walikuwa wanalalamika tukasema lazima tuweze ku ‘overcome’ yote haya, tutafute bora kwa nchi yetu. Sasa tumefika hapa tulipo” ameeleza.