Mbowe: Serikali na CCM ziliwasaidia Wabunge 19, ni uhuni usiovumilika

0
38

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe amesema kitendo cha kupeleka wabunge 19 ndani ya bunge ambao hawakutokana na maamuzi ya chama ni uvunjaji wa katiba na sheria na uhuni ambao haupaswi kuvumiliwa mahali popote na kwa mtu yeyote anayependa haki katika taifa.

Akizungumza katika kongamano la Siku ya Wanawake Duniani lililoandaliwa na Wanawake wa CHADEMA (BAWACHA) mkoani Kilimanjaro huku mgeni rasmi akiwa Rais Samia Suluhu Hassan Machi 08, 2023, amesema CHADEMA haijawahi kuridhia wabunge 19 kupelekwa bungeni kama baadhi ya taarifa zinavyovujishwa na baadhi ya vyombo vya habari.

Rais Samia: Siwezi kutia mkono suala la wabunge 19

“Sio kwa sababu tunawachukia wale wamama 19, wale walikuwa ni viongozi wetu, walikuwa ni sehemu yetu, walikuwa wamepigana na sisi, ni wanaharakati wenzetu, lakini walikengeuka. Na hao waliowasaidia kukengeuka ni watu walio kwenye serikali yako, ni watu walio katika chama chako, ni watu walio katika uongozi wa taasisi muhimu kama Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema.

Ameongeza kuwa “taasisi kama bunge ambalo linapaswa kutunga sheria linapaswa kuwa chombo safi, pamoja na kwamba kesi iko mahakamani, spika wa bunge anatambua vizuri sana kwamba tunavyozungumza leo hakuna zuio lolote la kimahakama linalowapa uhalali wabunge hao kubaki bungeni, wale wanajiwakilisha wenyewe na familia zao.”

Send this to a friend