Mbunge wa Viti Maalum, Hawa Mwaifunga amedai yeye na wenzake 18 hawakupewa nafasi ya kujieleza mahali popote kabla Baraza Kuu la CHADEMA halijapitisha uamuzi wa kuwapigia kura ya kuwafukuza uanachama.
Mwaifunga ambaye alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la CHADEMA (BAWACHA) ametoa madai hayo katika Mahakama Kuu Masijala Kuu mbele ya Jaji Cyprian Mkeha jijini Dar es Salaam.
Akijibu swali aliloulizwa na kiongozi wa jopo la mawakili wa CHADEMA, Wakili Peter Kibatala alipomuuliza kuwa muhtasari wa kikao cha Baraza hilo kilichofanyika Mei 11, 2022 unaonesha walipewa nafasi ya kusema chochote kabla ya wajumbe kupiga kura, Mwaifunga amedai nafasi pekee aliyopewa ilikuwa ni kuomba msamaha na siyo kusema chochote.
Jeshi la Polisi lakanusha madai ya CHADEMA
Ameongeza kuwa licha ya kupewa nafasi ya kuomba msamaha katika kikao cha Baraza, hakufanya hivyo kwa kuwa Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe kabla ya kuwaambia waombe msamaha alieleza tuhuma zao bila kuwapa nafasi ya kujitetea.
Aidha, amedai hakuridhishwa na kitendo cha Wajumbe wa Kamati Kuu kushiriki kupiga kura katika mkutano wa Baraza Kuu kwa kuwa wao ndio waliopitisha uamuzi wa kuwafukuza uanachama awali, uamuzi ambao ulizaa mkutano wa Baraza Kuu kujadili rufaa yao na baadaye kupigiwa kura za kufukuzwa uanachama.
“Mheshimiwa Jaji, Wajumbe wa Kamati Kuu ambao walikuwa 23 walikuwepo kupiga kura lakini ni wajumbe hao ndiyo walitufukuza kwenye mkutano wa tarehe 27 na hao hao walikuwepo kujadili na kufanya uamuzi kwenye mkutano wa Baraza Kuu,” amedai.
Ameongeza, “hivi isingewezekana hawa watu kukaa pembeni na kuacha wajumbe wa Baraza Kuu wafanye uamuzi bila wao kuwepo? Ni sahihi wao kusikiliza na kufanya uamuzi katika kikao cha Baraza Kuu?” amehoji.