Mbunge ashikiliwa kwa shambulizi dhidi ya waandishi wa habari Ngorongoro

0
44

Jeshi la Polisi Mkoa  wa Arusha linawashikilia watu kadhaa akiwemo Mbunge wa Ngorongoro, Emmanuel Ole Shangai kwa tuhuma za kuhusika na shambulizi dhidi ya waandishi wa habari lililotokea Ngorongoro mkoani humo.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha, Justine Masejo amesema baada ya kutokea kwa tukio hilo Agosti 18 mwaka huu katika eneo la Enduleni wilayani Ngorongoro, jeshi lilifanya uchunguzi  kuhusiana na tukio hilo na kufanikiwa kuwakamata watu hao.

Ameongeza kuwa, upelelezi wa tukio hilo tayari umekamilika na jalada limepelekwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa hatua za kisheria.

“Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha linatoa wito wa kuendelea kufuatwa kwa sheria, taratibu na kanuni za nchi ili kuweza kuhakikisha mkoa wetu unaendelea kuwa salama,” amesema Masejo.

Timu ya Waandishi wa habari na watumishi wa Serikali walijeruhiwa na vijana zaidi ya 200 wa jamii ya Kimasai (Morani) walipokuwa katika jukumu la utoaji elimu kwa wananchi waliojitokeza kujiandikisha kuhama kwa hiari katika Kijiji cha Enduleni kilichopo ndani ya eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kwenda Msomera wilayani Handeni.

Send this to a friend