Mbunge wa Iramba Mashariki, Francis Mtinga amesema bunge lina haja ya kutunga sheria ya kuwalinda wananchi kuhusiana na suala zima la matumizi ya bando ili kumuwezesha mtumiaji kutumia bando bila kikomo cha muda.
Ameyasema hayo bungeni jijini Dodoma wakati akichangia mapendekezo ya mpango wa maendeleo wa taifa wa mwaka 2023/2024 ambapo amemtaka Waziri wa Habari na mawasiliano kuwasilisha bungeni muswada huo ili kuwalinda wananchi na kuepusha kuibiwa na mitandao hiyo ya simu.
Waathirika wa ajali ya Precision Air kulipwa TZS bilioni 396
Kwa upande wake Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye wakati akijibu hoja hiyo amesema suala la bando za simu kuisha muda wake sio wizi kwa watumiaji bali ni utaratibu wa kawaida wa kibiashara uliowekwa na wala sio suala la kisheria.
“Bando ni huduma ya ziada ambayo ina masharti ya muda, ndiyo maana kuna bando la wiki, la mwezi na kuendelea. Ukitaka lisiishe kwa muda, upo utaratibu wakutumia ‘main tarrif’ ambayo ukiweka mpaka utakapoimaliza, hata kama ukikaa nayo kwa mwaka mzima,” amefafanua Waziri Nnauye.
Hata hivyo kuhusiana na ongezeko la bei ya vifurushi vya intaneti katika mitandao ya simu Serikali imesema ni kunatokana na marekebisho ya makosa yaliyofanyika.
Mtinga ametaka mabadiliko ya sheria yafanyike, ili mteja akijiunga kifurushi, kisiishe kutokana na muda, bali kiishe pindi yeye atakapomaliza kukitumia.