Mbunge Gambo amuomba Rais Samia kuingilia kati soko la Tanzanite

0
34

Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini Mrisho Gambo amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati suala la biashara ya madini ya Tanzanite kwa kuyaruhusu kuuzwa katika masoko yote ya madini nchi nzima ili rasilimali hiyo ya Taifa iweze kuwanufaisha watanzania wote.

Ameyasema hayo Oktoba 18, 2024 katika mkutano baina ya mbunge huyo na wafanyabiashara wadogo wa madini Arusha ambao wametoa hisia zao mbele ya mbunge huyo wakionyesha kutoridhika na madini ya Tanzanite kutouzwa katika soko huru.

“Nina imani kubwa na Rais Samia kwani ni kiongozi mpenda haki, anaamini kwenye biashara huria na anayependa watanzania wanufaike na rasilimali zao, hivyo hata katika suala la madini ya Tanzanite kuuzwa katika soko huru atashughulika nalo” amesema Mbunge Gambo.

Gambo amesema Madini ya Tanzanite ni madini yenye jina kubwa duniani cha kushangaza madini ya kutoka nchini DRC Congo yapo katika soko la madini mkoani humo lakini Tanzanite inayochimbwa katika mji wa Mererani mkoani Manyara haiwezi kuuzwa katika soko hilo mkoani humo.

Amesema toka kuasisiwa kwa katazo la madini hayo kuuzwa kiholela, thamani yake imezidi kuporomoka kwani kwa mujibu wa takwimu kutoka tume ya madini, mwaka 2017 – 2018 gramu 476,000 thamani yake ilikuwa shilingi bilioni 55, na mwaka 2022 – 2023 gramu milioni 23,000,015 thamani yake ni shilingi bilioni 56 jambo ambalo linaonyesha wazi kuwa kumekuwepo na anguko kubwa la bei ya madini hayo adimu duniani.

“Mnaweza mkaona kabisa hawa ambao wanataka kuyafungia madini ya Tanzanite wanalipeleka wapi taifa, kwa hiyo hili jambo kwani ni jambo ‘very serious’ hatuangalii ajira peke yake, siku za nyuma ukiacha hawa mabroker hapa pale kwenye jengo la PSSF lilikuwa limejaa, kulikuwa na mashine za kutosha watu wanakata madini leo hakuna kitu” amesema Gambo.

Gambo amesema kutokutoa uhuru wa kufanya biashara hiyo na kutengeneza sheria ambazo hazimlindi mfanyabiashara mdogo wa kati na mkubwa, kunasababisha utoroshaji wa madini hayo kwa njia ya panya, kuongezeka kwa ujanja ujanja pamoja na kuibuka kwa makundi ya ubabaishaji yasiyokuwa na lengo jema la kuyalinda madini hayo kwa wivu mkubwa.

Mbunge Gambo amesema furaha yake ni kuona madini ya Tanzanite yanauzwa nchi nzima bila kuwekewa vikwazo, kwani baada ya Serikali kutatua suala la leseni halitamsaidia mfanyabiashara kwani atakosa madini ya kuuzwa kutokana na zuio ama katazo lililopo linalotaka madini hayo kununuliwa Mererani na kuuzwa nje ya nchi pekee.