Mbunge January Makamba aeleza mambo 16 aliyojifunza kutokana na janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona

0
38

Orodha hii imenukuliwa na Swahili Times toka katika akaunti rasmi ya Mbunge wa Bumbuli, Januari Makamba kwenye mtandao wa Twitter, ambapo aliichapisha Aprili 2, 2020.

______

  1. Majanga na mitihani inatoa fursa ya kujifunza mambo mapya. Nimetumia janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona [COVID19] kujifunza masuala kadhaa (hasa ya virusi na maambukizi) kutoka kwenye maandiko ya kitaaluma na mazungumzo na wataalam. Napenda kuchangia niliyojifunza.
  1. Kwanza neno Corona. Corona ni neno la Kilatini. Tafsiri yake kwa Kiswahili ni taji. Corona hutumika zaidi kuelezea “taji la mwanga” linalovika au linalotokana na nyota, jua au mwezi. Jua linapozama, unaona jua na duara la mwanga linalozunguka jua. Hilo duara ndio Corona.
  1. Kwanini kuna virusi vimepewa jina hili? Kwasababu kuna familia kubwa ya virusi ambavyo ukivitizama kwenye microscope umbile lake linafanana na Corona. Virusi vya aina hii huruka kutoka kwenye wanyama (hasa popo) na kwenda kwenye binadamu), na sio lazima kwa kula wanyama hawa.
  1. Katika familia kubwa ya mamia ya virusi vya Corona, aina saba ndio “zimeruka” kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu. Kwahiyo, tukitafuta ufasaha, hakuna ugonjwa unaoitwa “Ugonjwa wa Corona”. Yapo magonjwa saba yanayosababishwa na aina moja au nyingine ya virusi vya Corona.
  1. Katika aina hizo saba, maarufu ni virusi vitatu: cha kwanza kilipewa jina la MERS-CoV (Middle-East Respiratory Syndrome coronavirus) kilichoibukia Saudi Arabia mwaka 2012 na kuenea nchi 27 na kusababisha ugonjwa wa mfumo wa kupumua (MERS) uliowapata watu 2600 na kuuwa watu 866.
  2. Kirusi cha pili cha Corona kilipewa jina la SARS-CoV-1 (Severe Acute Respiratory Syndrome coronavirus 1), kilicholipuka mwaka 2002 huko China na kuenea nchi 21 na kusababisha ugonjwa wa SARS unaoshambulia mfumo wa kupumua uliowapata watu 8,400 na kuua watu 813.
  1. Kirusi cha tatu maarufu cha Corona ni hiki tulichonacho sasa. Jina lake rasmi ni SARS-CoV-2. Kimeibukia China mwaka 2019 na kuenea nchi 180 hadi sasa na kusababisha ugonjwa wa mfumo wa kupumua uliopewa jina la COVID-19 uliowapata watu 943,000 na kuwaua watu 47,500 hadi sasa.
  1. Virusi vya SARS-CoV-1 na MERS-CoV vimedhibitiwa kwa sehemu kubwa ingawa bado hakuna tiba wala chanjo (kwa kudhibiti ueneaji wake) ingawa kwa asili havikuwa virusi vinavyoenea kwa haraka na kwa kasi. Virusi vya MERS-CoV vilikuwa hatari zaidi kwani 35% ya waliogua walifariki.
  1. Kirusi hiki tulichonacho sasa kinaenea kwa kasi zaidi kwasababu: wanaoambukizwa hawaonyeshi dalili kwa muda mrefu na wanavisambaza kwa wengi huku wakiwa wazima. Pia kirusi hiki kinadumu (hadi siku kadhaa) kwenye vitu mbalimbali tunavyovigusa mara kwa mara (meza, n.k).
  1. Kuhusu virusi kwa ujumla: Dunia hii ni ya virusi. Uzito wa virusi vyote duniani unazidi uzito wa binadamu. Hata hivyo asilimia kubwa ya virusi havina madhara. Hatari kubwa ya virusi ni kwamba bado hatujagundua vyote, na hatujui lini vipya vitalipuka na ukubwa wa madhara yake.
  1. Kihistoria, binadamu amekabiliwa na majanga ya virusi mbalimbali yaliyoua mamilioni lakini amevikabili kwa chanjo, tiba na ujenzi wa kinga. Mfano virusi vya Rubeola vinavyoleta surua, virusi vya Variola vinavyoleta ndui, nk. Kwahiyo matumaini ya tiba na chanjo ya COVID19 yapo.
  1. Lakini pia vipo virusi, kama vile HIV, vinavyosababisha UKIMWI, ambavyo tangu tuvijue miaka 35 iliyopita, pamoja na mabilioni ya dola kutafuta chanjo na tiba, hadi sasa hatujafanikiwa. Chanjo na tiba ya COVID19 inatafutwa kwa kasi, lakini hakuna uhakika wa mafanikio ya haraka.
  1. Virusi pia huwa vina tabia mahsusi ya kujibadilisha, yaani mutation, na hivyo kujenga sifa mpya za kimaumbile/kibaiolojia. Jambo hili hufanya kazi ya kuudhibiti maambukizi au kutafuta tiba au chanjo kuwa ngumu. Kasi ya kujibadilisha inatofautiana kati ya aina ya virusi.
  1. Dalili zinaonyesha kwamba kirusi hiki kinabadilika lakini sio kwa kasi kubwa. Mwisho, mambo mengi bado hayajajulikana kuhusu SARS-CoV-2 na COVID19, ikiwemo urahisi na uharaka wa aliyeambukizwa kuambukizwa tena akipona. Dawa kwa sasa ni kufuata maelekezo ya wataalam.
  1. Zaidi: virusi ni vidudu vijanja sana. Vina-evolve na kujibadilisha ili viweze kusambaa kwa urahisi zaidi, kuleta madhara makubwa zaidi, na kuhakikisha haviuawi. Kuna virusi vikiingia vinashambulia au kupumbaza kwanza mfumo wa kinga. Ndio maana mapambano na virusi ni makali.
  1. SARS-CoV-2 vikikuingia vinatulia kwenye koo kwanza ili ukikohoa vitoke na kufuata wengine. Ndo maana dalili ya kwanza ni kukohoa. Then vinajigandisha kwenye seli za mapafu na kujizalisha kwa mabilioni na kufanya mfumo wako wa kinga u-overheat kiasi kwamba hiyo tu inakuuguza.
Send this to a friend