Mbunge: Kuna uwezekano video 400 za Baltasar zimetengenezwa

0
59

Mwakilishi wa Wanawake wa Nairobi katika Bunge la Kenya, Esther Passaris, ameamsha mjadala mzito kuhusu matumizi ya akili bandia (AI) katika ulimwengu wa kisasa, akizungumzia kashfa inayomuhusisha Baltasar Engonga, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kitaifa la Upelelezi wa Kifedha (ANIF) la Guinea ya Ikweta.

Engonga amejikuta katika kashfa kubwa baada ya video zaidi ya 400 zinazodaiwa kumwonyesha akiwa na wanawake mbalimbali kuvuja mtandaoni. Ingawa wengi wameelekeza lawama kwake, Passaris amesema kwamba video hizo huenda zilitengenezwa kwa kutumia teknolojia ya AI.

Katika hotuba yake kwenye Bunge la Pan-Afrika lililofanyika Afrika Kusini, Passaris amegusia hatari zinazoweza kutokea kutokana na matumizi ya AI, na jinsi inavyoweza kuathiri haki za binadamu.

“Ninapotazama haki za binadamu na haki za watu, nahisi kwamba, pamoja na kuibuka kwa AI, tume inafanya nini kuhakikisha inalinda haki za watu? Haki nyingi zitaathiriwa ikiwa hatutakuwa na njia za kushughulikia sheria za AI,” amesema.

Kupitia kauli yake, Passaris ameangazia umuhimu wa kuanzishwa kwa sheria za kudhibiti matumizi ya AI ili kulinda faragha na haki za watu, akionyesha wasiwasi kuhusu madhara yanayoweza kutokea ikiwa watu binafsi wataendelea kuathiriwa na teknolojia hii bila kuwepo na udhibiti wowote.

Send this to a friend