Mbunge Silinde: CHADEMA wasiponidhamini kwenye uchaguzi, nitatumia chama kingine

0
24

Wakati idadi kubwa ya wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) hawahudhurii vikao vya Mkutano wa 19 wa Bunge unaoendelea jijini Dodoma, Mbunge wa Momba amekiuka msimamo wa chama chake.

David Silinde alipoulizwa sababu za kuhudhuria vikao licha ya wenzake kuazimia wasihudhurie amesema kwa waliomtuma bungeni ni wananchi na aliwaahidi atapambana hadi mwisho na sio kususa.

Kutokana na uamuzi huo mbunge huyo ameandika barua kwenda kwa mwenyekiti na katibu mkuu wa chama hicho akiwaleleza kuhusu uamuzi wake wa kujivua nafasi za uongozi.

“Nimemuandikia Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na katibu mkuu kuwa nimejiuzulu nafasi yangu ya Katibu wa Wabunge na Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani wa Wizara ya Viwanda na Biashara,” amesema Shilinde.

Shilinde amefikia uamuzi huo baada ya kushinikizwa na wabunge wengine, na amesema hawezi kukaa nje ya bunge wakati wananchi waliomtuma wakiwa na shida.

Aidha, ameongeza kuwa chama cha siasa ni mdhamini tu kwa mtu kuchaguliwa, hivyo kama hatopata udhamini wa CHADEMA, wananchi wa jimboni kwake watamchagua kwa chama kingine.

“Idhini ya mtu kufika bungeni ni wananchi na wala sio chama cha siasa. Chama cha siasa ni mdhamini tu, yani kama gari. Ukiamua kwenda Dar es Salaam kwa Shabiby, Kimbinyiko, au kitu chochote unaweza ukafika,” amesema mbunge huyo.

Pia amekosoa uamuzi wa chama chake kuzuia wabunge kuhudhuria vikao kwa hofu ya kuambukizwa virusi vya corona na kusema kuwa, baada ya siku 14 ambazo wabunge hao watakuwa nje (karantini) kumalizika, watarudi bungeni kuungana na wabunge ambao hawakuwa karantini, hivyo wanakuwa hawajatafuta suluhisho la tatizo.

Send this to a friend