Mbunge wa Chalinze aeleza kukerwa na migogoro isiyokwisha

0
32

MBUNGE Jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete ameeleza kukerwa kwake na migogoro isiyokwisha baina ya vijiji na vijiji kuhusu mipaka na ile ya wakulima na wafugaji ndani ya Chalinze.

Akizungumza katika mkutano wake uliofanyika Kata ya Kimange kushukuru na kupokea kero na maoni ya Wananchi uliofanyika Kijiji cha Pongwekiona na Kimange kwa nyakati tofauti, Mheshimiwa Mbunge alieleza jinsi migogoro hiyo inavyokwamisha juhudi za kuleta maendeleo jimboni hapo.

Akizungumza kujibu hoja iliyowasilishwa na wananchi, Mbunge aliwaagiza viongozi wa Serikali za vijiji hivyo kwamba ni lazima wasimamie sheria walizojiwekea ili kuondoa migongano isiyokwisha ikiwemo ile ya Wakulima na Wafugaji.

Ridhiwani ambaye pia kitaaluma ni Mwanasheria, alitumia nafasi hiyo kuwashauri wananchi na hasa Serikali za vijiji hivyo juu ya umuhimu wa kufuata sheria ili kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji na pia wanapotaka kujadili migogoro na vijiji vyengine.

Pamoja na kuwashauri huko kisheria, Mbunge alitumia nafasi hiyo ya ziara kuwaomba wananchi wamuunge mkono Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli katika juhudi zake za kuwakomboa wananchi wanyonge wa Tanzania katika ukandamizi unaofanywa na wachache wenye tamaa.

“Raisi wetu Magufuli anawashukuru sana kwa kura nyingi na amewaahidi kuwatumikia wananchi wake kwani mmeweza kumpatia ushindi wa kishindo wa zaidi ya asilimia 90.

Hivyo sisi kama wasaidizi wake jukumu letu ni kufanya kazi naye kuhakikisha nia yake inatimia na kwa kuanza tuanze kujikagua sisi wenyewe kama tunafanya yale aliyoyaelekeza .” Alisema Ridhiwani.

Aidha, katika ziara yake hiyo kero za migogoro ya baina ya wananchi jamii ya wafugaji na wakulima imeonekana kuwa kero katika Kata hiyo hivyo ameagiza kuendelea kusimamia sheria ikiwemo sheria za Vijiji na zile za Serikali kuu ili kuleta usawa baina ya pande zote mbili.

Aidha, mbali ya kero hiyo Wananchi wa Kijiji cha Pongwekiona walimuomba Mbunge wao huyo kusimamia maboresho ya barabara inayotoka Kimange-Pongwekiona ili iweze kupitika wakati wote bila shida.

Wakitoa kero zao hizo, wananchi hao walibainisha kuwa, wamekuwa wakipata vikwazo pindi wapatapo dharura ya mgonjwa ama mama mjamzito ili kumwaisha sehemu za huduma kama Kituo cha afya ama Hospitali ya Wilaya Chalinze.

“Mbunge wetu chondechonde wananchi wako huku Pongwekiona tunashida kubwa ya barabara haswa wakati wa masika hii barabara haipitiki na nadhani mmejionea wakati mnakuja huku.” Alisema Saumu Hamiss mkazi wa Pongwekiona.

Kwa upande wake Mwanawetu Salum alisema barabara hiyo imekua kero kubwa ikiwemo kushindwa kusafirisha bidhaa zao hoja ambayo iliungwa mkono na karibu wananchi wote katika mkutano huo.

Mbunge anaendelea na ziara katika Kata mbalimbali ikiwa ni muendelezo wa kukutana na wananchi kuwashukuru kwa kukipigia kura Chama Cha Mapinduzi CCM na kumpatia ushindi wa kishindo Mgombea wake Dkt. Magufuli na pia kujipanga katika kutekeleza Majukumu mara baada ya kuapishwa Baraza la Madiwani.

Mwisho.

Send this to a friend