Mchakato wa Hadhi Maalum kwa Diaspora kukamilika mwakani

0
42

Serikali imesema inatarajia kukamilisha utaratibu wa kuwapatia Hadhi Maalum Watanzania waishio nje ya nchi (Diaspora) ifikapo mwaka 2024.

Hayo yamesemwa katika hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na Diaspora wa Tanzania nchini Uholanzi kwa heshima ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba aliyepo nchini humo kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia tarehe 13 – 15 Novemba 2023.

Waziri Makamba amesema utekelezaji wa Hadhi Maalumu unategemea kufanyika kwa mapitio ya baadhi ya sheria za nchi kama ile ya ardhi na uhamiaji ili kurahisisha utekelezaji wenye tija kwa walengwa na mchakato huo unatajiwa kukamilika kabla ya kumalizika kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

“Miongoni mwa masuala yatakayopewa kipaumbele kwenye Hadhi Maalum ni haki ya kurithi au kurithishwa mali kwa diaspora wa Kitanzania aishiye nje ya nchi. Ili kutekeleza hili kuna maeneo ya sheria yetu lazima yabadilishwe ili watoto wenu wanaoishi huku nje waweze kurithi au kumiliki ardhi,” amesema.

Tanzania na Saudi Arabia zasaini mikataba ya ajira kwa Watanzania

Ameongeza kuwa “kwenye Hadhi Maalum, mtaruhusiwa kuja nyumbani na kukaa kwa muda mnaotaka bila malipo ya visa. Lakini kwanza ni lazima sheria yetu ya uhamiaji ipitiwe na kurekebishwa, ili kuruhusu kurudi nyumbani bila kulipishwa visa.”

Aidha, ameeleza kuwa baadhi ya masuala mengine yatakayowanufaisha watumiaji wa Hadhi Maalum ni fursa na motisha mbalimbali za kuwekeza nchini Tanzania kupitia Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC).

Send this to a friend