Mchanganuo wa ajira 32,000 zilizotangazwa leo na serikali

0
59

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama ametangaza ajira mpya zaidi ya 32,000 katika sekta za ualimu, afya, kilimo, mifugo, uvuvi na maji huku watumishi 92,000 wakipandishwa vyeo na 6026 wakibadilishiwa kada.

Katika sekta ya ualimu imetoa ajira 12,035 ambapo nafasi 9,800 kwa ajili ya walimu wa shule za msingi na sekondari, afya nafasi 10,285 zinazojumuisha nafasi 7,612 kwa ajili ya hospitali, vituo vya afya na zahanati zilizopo katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Waziri Mhagama amesema Serikali imeamua kutekeleza ahadi yake ya kuajiri watumishi wengine 32,604 kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha na mchakato wa ajira hizi unaanza leo.

“Niseme tu taarifa hii ni hatua ya kwanza ya mchakato wa kuhakikisha utekelezaji wa ajira hizo unakamilika kabla ya mwaka wa fedha 2021/22 haujaisha. Utekelezaji wa ajira hizi utaigharimu Serikali kiasi cha shilingi bilioni 26.3 kwa mwezi sawa na shilingi bilioni 315.6 kwa mwaka,” amesema.

Aidha Waziri Mhagama ameziagiza Mamlaka za Ajira, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Wizara ya Afya pamoja na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kuhakikisha wanaendesha michakato ya ajira kwa uwazi, weledi, uadilifu.

Send this to a friend