Mchungaji aamriwa kumrudishia muumini fedha alizodai ni fungu la 10

0
40

Mahakama Kuu ya Tanzania Masijala ya Dar es Salaam imetolea uamuzi mgogoro baina ya mchungaji John Mtuka wa Kimara na muumini wake, Neema Wawa juu ya fedha alizomkopesha mchungaji huyo ambaye amedai kuwa zilikuwa ni sadaka ya fungu la 10, na kubainisha kuwa zilikuwa ni mkopo hivyo zinapaswa kurejeshwa.

Muumini huyo alimfikisha Mchungaji Mtuka katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni akidai shilingi milioni 15 alizomkopesha, na mahakama hiyo ilimpa ushindi Neema Agosti 2, mwaka huu, hivyo kupelekea mchungaji huyo kukata rufaa Mahakama Kuu.

Jaji wa Mahakama Kuu, John Nkwabi amesema kulingana na ushahidi wa pande zote mbili, mchungaji alibaini muumini huyo alikuwa na fedha za kutosha kwenye akaunti, akaanza kumwomba amkopeshe ambapo mwanzoni muumini huyo alikataa lakini kutokana na mchungaji kuapa kuwa angemrudishia, alimkabidhi TZS milioni 15 kama mkopo ambao haukuwa na riba.

“Wakati mchungaji anadai muumini wake alilipa shilingi milioni tano kama fungu la 10, muumini wake anasema alilipa tu shilingi milioni moja kama fungu la 10. Kwa maoni yangu, utata wa hii kesi ulianzia hapa, ukichanganya na madai ya michango ya ujenzi,” amesema.

Kwa upande wa mchungaji huyo, amedai Mahakama ya Kinondoni haikuzingatia mahusiano yaliyopo kati ya mchungaji na muumini, na kwamba Neema alikuwa muumini wa kanisa hilo, ilimfanya awajibike kulipa sadaka ya fungu la 10 na kutoa michango mbalimbali ya kanisa kabla ya kubadilika na kuanza kudai arejeshewe.

Jaji Nkwabi amemwamuru Mchungaji Mtuka kumlipa muumini huyo TZS milioni 13.9 pamoja na kulipa gharama za shauri hilo katika mahakama kuu na mahakama ya wilaya.

Send this to a friend