Mchungaji Msigwa adai Sugu hakushinda kihalali, akata rufaa

0
68

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Nyasa, Mchungaji Peter Msigwa ambaye ameshindwa kwenye uchaguzi uliompa ushindi Joseph Mbilinyi maarufu Sugu, amekata rufaa kupinga matokeo ya uchaguzi akidai kuwa uchaguzi huo ulivurugwa.

Hayo ameyasema Juni 03, 2024 wakati akizungumza na waandishi wa Habari ambapo amesema uchaguzi huo uligubikwa na mbinu chafu ikiwa ni pamoja na makatibu watatu wa mabaraza kuzuiliwa kupiga kura na wasimamizi wa uchaguzi pamoja na kumpa ushindi ambaye hakustahili, jambo ambalo ni kinyume na katiba ya chama hicho

“Nimekata rufaa kwa chama changu kwamba ushindi ule haukuwa halali na kulikuwa na mbinu chafu. Kama CHADEMA tunalalamikia CCM kwamba wasimamizi wa uchaguzi huwa hawatendi haki, CHADEMA tulitakiwa tuwe mfano, sasa kama mimi mjumbe wa Kamati Kuu ninatoa malalamiko hayasikilizwi tena ndani ya chama chenye kutenda haki nani atasikilizwa katika nchi yetu?” amesema.

Ameongeza, “haya malalamiko sijaanza leo baada ya uchaguzi, nimelalamika ndani ya vikao vya Kamati Kuu, nimetuma barua kwa Katibu Mkuu nimezungumza na hata siku mbili kabla ya uchaguzi nimelalamika kwamba kuna mambo ambayo hayako sawa.”

Aidha, Msigwa amesema alikuwa akifanya kampeni za wazi, zenye ushindani na uaminifu mkubwa lakini mgombea mwenzake alikuwa na nguvu nyingine nyuma yake, jambo ambalo ni hatari kwa demokrasia.

Mchungaji Msigwa alishindwa uchaguzi huo baada ya kupata kura 52 sawa na asilimia 49.05 huku mshindani wake Joseph Mbilinyi akishinda kwa kura 54 sawa na asilimia 50.90 za kura.

Send this to a friend