Mdee na wenzake wafungua kesi ya kupinga kufukuzwa CHADEMA

0
48

Baada ya mahakama kutoa kibali kwa waliokuwa wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Halima Mdee na wenzake 18, sasa wamefungua shauri la kupinga kuvuliwa uanachama wa chama hicho.

Mahakama ilitoa kibali cha kufungua shauri hilo Julai 8, mwaka huu baada ya kukubaliana na hoja zao katika maombi waliyokuwa wameyafungua wakiomba ridhaa hiyo.

Mawakili wa Mdee, Ipilinga Panya na Aliko Mwamanenge wameieleza Mwananchi kuwa, walifungua shauri hilo jana Alhamisi Julai 21, 2022 mpaka sasa shauri hilo limeshasajiliwa baada ya nyaraka walizoziwasilisha mahakamani hapo kufanyiwa ukaguzi na mahakama kujiridhisha kuwa zimekamilika na taratibu zimefuatwa kwa mujibu wa sheria.

Aidha, katika shauri hilo la maombi ya mapitio ya mahakama, Mdee ambaye alikuwa mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa CHADEMA (BAWACHA) na wenzake wanapinga uamuzi wa kufukuzwa uanachama uliotolewa na Baraza Kuu la Chadema Mei 11, 2022.

Katika uamuzi huo, Baraza hilo lilitupilia mbali rufaa zao walizozikata wakipinga uamuzi wa awali wa kuwavua uanachama uliotolewa na Kamati Kuu ya Chadema Novemba 27, 2020. Badala yake Baraza hilo liliunga mkono uamuzi huo wa Kamati Kuu.

Baada ya kukamilisha hatua hiyo ya kufungua shauri hilo, sasa wanasubiri taratibu nyingine za kimahakama ikiwa ni pamoja kupangiwa jopo la majaji watakaosiliza shauri lao hilo na tarehe ya kutajwa na kisha tarehe ya usikilizwaji baada ya taratibu zote kukamilika.

Chanzo: Mwananchi.

Send this to a friend