Mei Mosi: Rais Magufuli awaambia wafanyakazi corona isizuie kazi
Rais Dkt. John Pombe Magufuli amewapongeza na kuwatakia heri Wafanyakazi wote hapa nchini ambao leo tarehe 01 Mei, 2020 wanaadhimisha Siku ya Wafanyakazi (Mei Mosi).
Mwaka huu sherehe za Mei Mosi hazitafanyika ili kuepusha mikusanyiko ya watu, ikiwa ni hatua muhimu ya kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona (Covid-19).
Rais Magufuli amesema licha ya kwamba sherehe za Mei Mosi hazitafanyika mwaka huu, serikali inatambua mchango mkubwa unaotolewa na wafanyakazi katika ujenzi wa taifa na itaendelea kusimamia maslahi yao na kuboresha mazingira ya kazi.
Amewataka wafanyakazi hao kuendelea kuchapakazi kwa juhudi na maarifa ili Watanzania waendelee kunufaika na huduma wanazozitoa katika maeneo yao ya kazi huku wakichukua tahadhari zote zinazoelekezwa na wataalamu juu ya kujikinga na ugonjwa wa Corona.
“Ndugu wafanyakazi wenzangu nawapongeza sana kwa kuchapa kazi, mimi nipo pamoja nanyi na natambua kazi nzuri mnayoifanya, nawaomba katika kipindi hiki ambacho dunia inapita katika wakati mgumu wa kukabiliana na ugonjwa wa Corona, sisi tuendelee kuchapakazi, kamwe ugonjwa huu usiwe sababu ya kurudi nyuma na kuacha kuwahudumia Watanzania, mimi naamini Mwenyezi Mungu atatuvusha” amesisitiza Rais Magufuli.
Aidha, amewapongeza waajiri wote wa serikali na sekta binafsi, na ametoa wito kwao kutotumia ugonjwa wa Corona kama kigezo cha kuwanyanyasa wafanyakazi.