Membe atoa wito kwa wagombea na viongozi wa dini kuelekea uchaguzi
Wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 28 mwaka huu wametakuwa kukubali matokeo yatakayotangazwa, kwani hilo ni msingi katika kuhakikisha amani na utulivu unakuwepo.
Hayo yamesemwa na mgombea Urais wa Tanzania kupitia chama cha ACT-Wazalendo, Bernard Membe wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam ambapo ameongeza kuwa, kigezo cha nchi kuwa na amani, ni kutendeka kwa haki.
“Vyama vikubali matokeo [ya uchaguzi], hiyo ndiyo haki ya kwanza Watanzania wanaitaka.”
Aidha, amewataka viongozi wa dini kutojiingiza kwenye siasa badala yake waombee nchi na kuhubiri amani na utulivu wakati wote ili kuhakikisha umoja wa nchi katika kipindi chote.
“Ninawaomba viongozi wote wa kidini watushabikie kimya kimya kwa sababu ni rahisi kuiingiza nchi kwenye vita ya kidini. Dini mbili tofauti zinpowaunga mkono wagombea wa wili, vita inahama kutoka kwa wagombea kwenda kwenye dini, na vita vya dini haviishi.
Viongozi wa dini mna kazi mbili kubwa. Kuhubiri amani, haki na utulivu na kuliombea Taifa.”
Membe amesema sababu kubwa iliyomfanya agombee Urais ni kuimarisha diplomasia ya kimataifa kati ya Tanzania na jumuiya za kikanda na kimataifa.