Meneja: Hatuna taarifa ya Mwakinyo kuvuliwa ubingwa wa ABU

0
41

Uongozi wa bondia Hassan Mwakinyo umesema hauna taarifa rasmi kuhusiana na bondia huyo kuvuliwa ubingwa wa African Boxing Union (ABU) hivi karibuni.

Meneja wa bondia huyo, Huzeifa Manuari amesema kuwa ABU haijawaeleza chochote kuhusiana na jambo hilo na huenda kuna mkono wa mtu umehusika ili Mwakinyo avuliwe ubingwa.

“Ubingwa wa WBF ilitokea shida kidogo na promota ndiyo sababu Mwakinyo hakuutetea, ila huu wa ABU huenda kuna mtu nchini amehusika baada ya kuona Mwakinyo amekwenda Marekani kwenye programu zake nyingine, ngumi zetu zina mambo mengi,” alisema Huzeifa.

Meneja amesema kuvuliwa kwa mkanda huo haumuathiri bondia wake, kama ingekuwa mikanda mikubwa ya WBA, WBC au WBO ambayo ni mikanda mikubwa duniani ndiyo ingewatikisa, kwa kuwa point [alama] ziko palepale, na kwamba kilichopo ni kujipanga jinsi gani anaongeza alama na kuifikia nyota tano kutoka nne.

Hivi karibuni Katibu wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC), Yahaya Poli alifafanua utaratibu wa ABU kuwa bondia anapaswa kutetea ubingwa ndani ya miezi sita, kipindi hicho kikipita bila kutetea mkanda anavuliwa ubingwa.

Mtanzania Mwakinyo amepoteza taji hilo baada ya miezi saba kupita tangu aliposhinda mkanda Septemba mwaka jana.

Send this to a friend