Mfahamu Askofu Wolfgang Pisa, Rais mpya wa Baraza la Maaskofu Katoliki

0
92

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limemchagua Askofu Wolfgang Pisa kuwa Rais mpya wa baraza hilo.

Askofu Pisa ni Askofu wa jimbo Katoliki la Lindi anayechukua nafasi ya Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya, Askofu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga ambaye amemaliza muda wake.

Safari ya utawa ya Askofu Wolfgang Pisa;

Askofu Pisa alizaliwa tarehe 6 Julai mwaka 1965, Karatu, Jimbo Katoliki la Mbulu akiwa mtoto wa kwanza kati ya watoto nane.

Mwaka 1983 hadi mwaka 1986 alipata elimu yake ya Sekondari kuanzia kidato cha kwanza hadi cha Nne Maua Seminari kisha kuendelea na masomo yake ya kidato cha Tano na Sita kabla ya kwenda jeshini.

Askofu Pisa alianza safari yake ya utawa mwaka 1990 alipojiunga na Shirika la Ndugu Wadogo Wafransisko Wakapuchini (Order of Friars Minor Capuchin).

Baada ya masomo na malezi ya kitawa Lusaka, Zambia na Chuo Kikuu Kishiriki cha Jordan, Morogoro, mnamo Agosti 15, 1998, aliweka nadhiri za maisha na kuwa mwanachama kamili wa shirika hilo, hatua iliyomwandaa kwa huduma ya muda mrefu katika maisha ya kitawa.

Mwaka mmoja baadae, Septemba  Mosi mwaka 1999, Wolfgang Pisa alipata daraja takatifu ya upadre. Katika nafasi hii, alifanya kazi kwa bidii akitoa huduma za kiroho na kijamii kwa waumini na jamii kwa ujumla.

Hatua kubwa zaidi katika maisha yake ya kichungaji ilikuja Aprili 9, 2022, ambapo aliteuliwa kuwa Askofu wa Jimbo la Lindi, Tanzania. Alisimikwa rasmi kama Askofu wa Lindi tarehe 26 Juni 2022, hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kidini na kijamii, ikionyesha heshima na imani waliyonayo kwake.

Kama Askofu wa Lindi, Askofu Pisa amejitahidi kuimarisha maadili na kukuza imani miongoni mwa waumini wake. Ameweka msisitizo mkubwa katika elimu, afya, na maendeleo ya kijamii, akihakikisha kwamba kanisa linachangia kikamilifu katika ustawi wa jamii.

Hivi karibuni, Askofu Wolfgang Pisa amechaguliwa kuwa Rais mpya wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC). Nafasi hii muhimu inaashiria imani kubwa waliyonayo maaskofu wenzake na Kanisa Katoliki kwa ujumla juu ya uongozi na hekima yake.

Kama Rais wa TEC, anatarajiwa kuendeleza mshikamano, kuimarisha maadili, na kuongoza kanisa katika nyanja mbalimbali za kiroho na kijamii.

Send this to a friend