Mfahamu Hayati Mansoor Daya, mwanzilishi wa kiwanda cha kwanza cha dawa nchini

0
64

Mwanzilishi wa kwanza wa kiwanda cha dawa nchini Tanzania na Afrika Mashariki, Mansoor Daya alifariki dunia jana jijini Dar es Salaam.

Hadi kifo chake, Daya alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mansoor Daya Chemicals Limited iliyopo jijini Dar es Salaam ambayo imekuwa ikizalisha bidhaa za dawa nchini Tanzania kwa zaidi ya miaka 60.

Mansoor Daya ni nani hasa?

Kwa miaka mingi, Tanzania ilikuwa ikitegemea uagizaji mkubwa wa dawa kutoka nje, lakini Daya hakukubaliana na hali hiyo, aliamini kwamba Tanzania inaweza kujitosheleza katika uzalishaji wa dawa na hivyo kupunguza utegemezi wake kwa nchi za nje.

Mwaka 1962, Mansoor Daya alianzisha kiwanda cha dawa cha kwanza nchini Tanzania na hata katika Afrika Mashariki. Safari ilikuwa ngumu na alihitaji kuvunja vikwazo vingi vya kiuchumi na kisheria.

Kwa miaka mingi, kiwanda chake kilikua kwa kasi, kuzalisha dawa za ubora na kusambaza kote nchini na hata nchi jirani. Bidhaa zake zilikuwa zenye thamani na zilipatikana kwa bei nafuu, hivyo kufanya upatikanaji wa matibabu kuwa rahisi kwa wananchi.

Hapo awali kiwanda chake kilitengeneza dawa nne tu, tembe za aspirin, chloroquine, aspirin phenacetin caffeine compound na Vitamin B complex tablet.

Kwa sasa, kiwanda chake kinaweza kutengeneza zaidi ya tablet milioni 3 kwa kutumia mashine za kisasa na dawa hizo zinatolewa kwa Idara ya Bohari ya Dawa (MSD), hospitali na zahanati inayomilikiwa na serikali nchini Tanzania.

Mansoor Daya hakuridhika na mafanikio hayo, aliendelea kuhamasisha maendeleo na uvumbuzi katika kiwanda chake kwa kuongeza uzalishaji wa dawa mpya na hata kuanzisha dawa za mimea ili kufanya matibabu yawe nafuu zaidi kwa watu wa kawaida.

Leo hii Mansoor Daya hayupo tena, lakini urithi wake unaendelea kuishi. Tanzania inazidi kujikita katika uzalishaji wa dawa na afya, na mchango wa Mansoor Daya katika safari hii hautasahaulika kamwe.

Send this to a friend