Mfahamu kiongozi wa mapinduzi ya kijeshi ya Burkina Faso, Paul Damiba

0
57

Mara nyingi mapinduzi wa kijeshi yanapofanyika huwa ni mwisho wa uongozi ambao uliingia madarakani kwa njia ya kidemokrasia, na kuwa mwanzo wa utawala wa kijeshi.

Burkina Faso imekuwa nchi ya hivi karibuni zaidi Afrika kuripotiwa kufanya mapinduzi ya kijeshi na kuhitimisha uongozi wa Rais Roch Kabore ambao unadaiwa kwamba pamoja na mambo mengine, ulikuwa dhaifu katika kupambana na magaidi.

Mapinduzi hayo yanamuweka Paul-Henri Sandaogo Damiba kuwa kiongozi wa serikali ya mpito ambayo itaongozwa na wanajeshi.

Hadi kufikia wakati wa kufanya mapinduzi hayo Damiba alikuwa katika ngazi ya Luteni Kanali wa jeshi, na kiongozi wa ulinzi wa mji mkuu wa nchi hiyo Ouagadougou.

Alianza kutumikia nafasi hiyo Desemba 2021 baada ya kupewa wadhifa huo na Rais aliyepinduliwa, hatua ambayo wachambuzi walisema kuwa ulikuwa ni mkakati wa kutaka kuendelea kuungwa mkono na jeshi.

Kutoka kuwa mkuu wa usalama wa mji huo, mapinduzi yalipofanyika Januari 24 alitangazwa kuwa kiongozi wa Patriotic Movement for Safeguard and Restoration (MPSR).

Kwa mujibu wa Reuters, Damiba alipata mafunzo ya kijeshi nchini Ufaransa na kupata Shahada ya Umhiri katika Sayansi ya Jinai (Master’s Degree in Criminal Science) kutoka National Conservatory of Arts and Crafts (Conservatoire national des arts et métiers).

Hii haikuwa mara ya kwanza jina lake kutajwa katika masuala ya mapinduzi, kwani alikuwa shuhuda wa mapinduzi ya mwaka 2015 ambapo alikuwa sehemu wa mashihidi waliofika mahakamani kutoa ushahidi dhidi ya mtuhumiwa wakati huo.

Aidha, ni mwandishi ambapo kitabu chake kilichopewa jina la ‘West African Armies and Terrorism: Uncertain Responses kilichozinduliwa Juni 2021.

Damiba alikuwa kwenye televisheni wakati Kader Quedraogo akitangaza kuwa serikali imeondolewa na katiba imesimamishwa. Alisema kuwa karibuni jeshi litatangaza lini na kwa namna gani nchi itarejea kwenye utawala wa kiraia.

Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa kwa haraka ni kufungwa kwa mipaka na marufuku ya kutotoka nje nyakati za usiku.

Kufuatia mapinduzi hayo, Rais Kabore amepelekwa kwenye kambi ya jeshi ambako anashikiliwa.

Licha ya jeshi kusema kwamba mapinduzi hayo yamefanyika pasi na vurugu, Januari 23 mwaka huu wanajeshi na wafuasi wa serikali walirushiana risasi karibu na makazi ya Rais.

Licha ya serikali kukanusha, Jumatatu kulikuwa nchi hiyo ikiwa chini ya jeshi. Uamuzi huo wa jeshi unaaminika kwamba umetokana na kuzorota kwa hali ya usalama nchini humo.

Mwaka jana Rais aliyepinduliwa alichukua jukumu la kuwa Waziri wa Ulinzi, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kukabiliana na vitendo vya kigadi.

Send this to a friend