Mfahamu Rais mdogo mwanamke anayetarajiwa kufanya ziara Tanzania

0
54

Rais wa Hungary, Katalin Novák anatarajiwa kuwasili nchini Jumatatu, Julai 17 hadi 20, 2023 kwa ajili ya ziara ya kiserikali ya siku tatu kwa mwaliko wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Katika ziara hiyo, Rais Katalin atafanya mazungumzo na Rais Samia Suluhu Ikulu siku ya Jumanne hususani katika upande wa diplomasia, uchumi na biashara.

Krisztina Novák amezaliwa Septemba 06, mwaka 1977 ambapo alianza kazi yake katika utumishi wa serikali ya Hungary mwaka 2001 akihudumu katika Wizara ya Mambo ya Nje na kubobea katika masuala ya Umoja wa Ulaya na Ulaya kwa ujumla.

Mnamo mwaka 2010, alihudumu kama Mshauri wa Wizara ya Mambo ya Nje, na mnamo mwaka 2012 aliteuliwa kuwa Mkuu wa Baraza la Mawaziri la Wizara ya Rasilimali Watu.

Mwaka 2014, alikuwa Katibu wa Jimbo katika Masuala ya Familia na Vijana. Akiwa kama mwanachama wa chama cha Fidesz, Novák pia amehudumu kama mbunge katika Bunge la nchi hiyo kuanzia mwaka 2018 hadi 2022, na kama Waziri wa Masuala ya Familia katika Serikali ya nne ya Orbán kuanzia 2020 hadi 2021.

Rais Novák alichaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Hungary mwaka 2022 akiwa na umri wa miaka 45, ndiye Rais mwenye umri mdogo zaidi kuwahi kuongoza nchi hiyo, pia mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo.

Send this to a friend