Mfahamu Theresa Ntare, Chifu wa kwanza mwanamke Tanzania

0
99

Alipata nafasi ya kwenda kusoma Ulaya enzi ukoloni nafasi maalum za watoto wa machifu. Alihitimu mafunzo ya ya sheria akawa msaada mkubwa sana wa kisheria wakati wa kudai uhuru, hasa kwenye mikataba ya kimataifa.


Mengi hayajulikani katika historia ya utoto wa Mwami Theresa Ntare, lakini inaaminika alikuwa mtoto wa kike pekee wa Chifu Ntare. Inaelezwa kwamba Mwami Theresa Ntare alitawazwa uchifu baada baba yake Mwami Ntare kukosa mtoto wa kiume. Baada kutawazwa uchifu ilibidi atafutiwe mchumba kutoka ukoo wa Chifu Lusimbi wa Kalinzi hivyo akawa ameolewa na kijana wa kitutsi kutoka Kalinzi akiitwa George Shinganya.

Kulingana na mila za Kiha, Mwami haolewi. Akiolewa inabidi ahame milki yake ya uchifu ili akawe mke wa huyo mwoaji. Hivyo basi, Mwami Ntare hakuolewa na George Shinganya. Bali familia ya Mwami ndiyo iliyolipa mahari kwa familia ya Shinganya. Hivyo, Jina la Shinganya likaondolewa na akaitwa George Ntare.

Baadaye ndoa ya Ntare na George ilivunjika na Mwami akaoana na Mwami Louis Dantes Ngua wa Ufipa(Huyu ana asili ya uchifu wa Ufipa). Kuna nadharia zinazoeleza pia kuwa Mwami Theresa Ntare alipata pia kuwa mke wa Chifu Makwaia wa Usukuma. Lakini hakuna ushahidi wowote juu ya hilo.

Wakati wa zama hizo jamii nyingi za Kiafrika zilitajwa kuwaweka nyuma wanawake hasa katika masuala ya Uongozi. Hilo halikumfanya Mwanamama Ntare asiweze kuongoza vizuri na kishupavu jamii yake ya Waha wa Heru huko Kasulu.

Hakuishia hapo, mama huyu aliweza kushika wadhifa mkubwa ambapo alikuwa ni Mkuu wa machifu wote Tanganyika akipokea kijiti kutoka kwa Chifu Petro Itosi Marealle mwaka 1958. Makabidhiano yalifanyika shule ya sekondari ya Mzumbe, na mpaka sasa Mzumbe kuna bweni linaitwa Ntare.

Mwani Theresa Ntare aliheshimika kama Chifu wa Kasulu yote na sio tu Heru alisimamia vyema msimamo wa Baraza la Machifu mwaka 1958 na kuunga mkono juhudi za TANU katika kudai uhuru.

Mwami Theresa Ntare alikuwa ni mmoja ya wabunge wachache wa Baraza la Kutunga Sheria la Tanganyika kabla hata ya Uhuru wa Tanganyika.

Aliendelea kuwa Mbunge mpaka miaka ya 1980, lakini kabla ya hapo aliachia uchifu Disemba 9, 1962, Katika Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam nchini Tanganyika. Hapo alikaribishwa kama Malkia wa Heru kwa Ngoma Maalum kutoka Ngome ya Malkia wa Heru kwa heshima kubwa.

Inaelezwa alifariki miaka ya 1990 na mara ya mwisho alikuwa akiishi maeneo ya karibu na barabara inayoelekea Munyegera – Kati ya ilipo shule ya msingi na Kahaga Dispensary (kulikuwa na soko hapo kati miaka ya 1985).

Kwa sasa Mwami wa Heru ni Costa Shinganya au Ntare ambaye ni mtoto wa kwanza wa Mwani Theresa Ntare.

Kuna wanaosema Mbunge wa Kigoma mjini, ndugu Zitto Ruyagwa Kabwe ndiye hasa Mwami wa Waha wote. Lakini hili ieleweke yeye amepewa heshima tu ya Mwami Mpole aliyejulikana kama Ruyagwa.

Huyu ndiye Mwami Theresa Ntare VI, Malkia wa Heru kuanzia 16 Aprili, 1946 mpaka 9 Novemba, 1962.


Matukio mawili yaliyowatokea yeye na Baba wa Taifa ni: Walizaliwa mwaka mmoja 1922,wamefariki mwaka mmoja1999.