Mfalme Zumaridi ahukumiwa mwaka mmoja jela

0
67

Diana Bundala maarufu ‘Mfalme Zumaridi’ amehukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela na Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Mwanza baada ya kumkuta na hatia katika makosa mawili kati ya matatu kwenye kesi ya jinai namba 10/2022.

Akisoma hukumu hiyo leo Januari 25, 2023 Hakimu Mfawidhi wa Mahakama, Monica Ndyekobora amesema Zumaridi na wenzake wanne wamekutwa na hatia katika makosa mawili ambayo ni pamoja na kumzuia Ofisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Nyamagana, Christina Mwisongo (46) kutekeleza wajibu wake na kuzuia maofisa wa polisi kutekeleza jukumu lao.

Isome hapa ripoti ya Wizara ya Afya kuhusu watumishi walioonekana kwenye video wakizozana

Aidha, pamoja na makosa hayo, Hakimu Ndyekobora hajawakuta na hatia katika kosa la shambulio la kudhuru mwili huku washitakiwa wengine watatu wakiachiliwa huru.

Hata hivyo Zumaridi atatumikia mwezi mmoja katika gereza la Butimba jijini Mwanza kutokana na kukaa miezi 11 mahabusu wakati kesi hiyo ilipokuwa inasikilizwa, huku wenzake wanne wakitumikia kufungo cha nje.