Mfumo wa LIPA wa Vodacom M-Pesa unaleta mapinduzi katika mifumo ya malipo Tanzania

0
42

Dar es salaam: Kampuni ya mawasiliano ya simu inayoongoza Tanzania, Vodacom Tanzania PLC leo imezindua huduma yake ya LIPA KWA SIMU katika gulio la M-pesa lililofanyika Mlimani City Mall jijini Dar es salaam. Gulio hilo lina lengo la kuongeza ufahamu wa upana wa huduma za kifedha zinazotolewa na mfumo wake mpya wa malipo.

Akiongea wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi wa M-Pesa Epimack Mbeteni alisema kwamba Vodacom Tanzania iliona hitaji la kupanua mfumo wa LIPA kwa M-Pesa kutoka katika mfumo wa M-Pesa, na  kuanza kupokea malipo kutoka mitandao na benki zote na kufikia katika kuwezesha malipo ya kidijitali katika mifumo ya rejareja na manunuzi mitandaoni.

Amesema kwamba Vodacom imezindua huduma ya “Lipa Kwa Simu” kuhamasisha matumizi ya mifumo ya malipo ya kidijitali kama njia kuu ya malipo nchini, na kuhama kutoka katika utegemezi mkubwa wa fedha taslimu uliopo sasa.

“Lipa kwa Simu ni hatua ya kimapinduzi iliyochukuliwa na kampuni ya Vodacom kuelekea katika kujenga jamii isiyotumia fedha taslimu kwa kusaidia ushirikiano wa malipo katika mitandao na benki zote.  Kwa kutumia huduma ya Lipa kwa Simu, wafanyabiashara na wamiliki wa biashara wanaweza kupokea malipo kutoka katika mitandao na benki zote na kuongeza ufanisi na usalama katika biashara zao.  Na kwa upande wa wateja, bila kujali unatumia mtandao gani, sasa unaweza kufanya malipo kupitia mfumo wa LIPA kwa kutumia gharama za kawaida za kuhamisha fedha. Jambo ambalo linaondoa mahitaji ya kutembea na kiasi kikubwa cha fedha taslimu,” alisema Mbeteni.

Vodacom imewezesha LIPA kwa Simu kwa makundi mbalimbali ya wafanyabiashara wa sekta zote kama Baa, Hoteli, migahawa, Supamaketi, Vituo vya mafuta, kumbi za sinema, maduka ya dawa, Maduka ya vifaa vya ujenzi na kadhalika kwahivyo inapatikana kote.

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa kodi wa TRA, Richard Kayombo ameipongeza huduma hii inayotolewa na M-Pesa na kusema kwamba imerahisisha na kuleta ufanisi katika mifumo ya malipo ya Umma kwa sababu sasa wateja wanaweza kulipia bili, tozo na huduma nyingi za kijamii kupitia mfumo huu wakiwa sehemu yeyote ile, iwe nyumbani au maeneo yao ya kazi. 

“Serikali inajivunia kuwa mshirika katika huduma ya fedha kupitia simu za mkononi, kwa sababu watu wanaweza kufanya malipo kwetu. Iwe katika mifumo ya mahakama za manispaa, polisi au huduma za afya na nyinginezo.  Jambo hili limeongeza uwazi na hali ya kukidhi taratibu za malipo kwa jamii,” aliongeza Kayombo.

Gulio la M-Pesa lililofanywa na kampuni ya Vodacom lilivutia maelfu ya wateja, wafanyabishara na jamii kwa ujumla ambao walikuja kujifunza na kuona jinsi ambavyo mfumo mpya wa Lipa kwa Simu umerahisisha huduma ya malipo nchini.

Kwa upande wake, Bi Mwajuma Hamisi amesherehekea mfumo wa Lipa kwa Simu akisema kwamba ni mfumo ambao utaleta mabadiliko kwa kuwa hakutakuwa na haja tena ya kutembea na kiasi kikubwa cha fedha au kulipia gharama za miamala za kuhamisha fedha kutoka benki kwenda katika simu za mkononi. 

“Nimenunua vipodozi na vitu vingine kutoka kwa wafanyabiashara mbalimbali hapa katika gulio na nilichofanya ni kuscan msimbo wa majibu ya haraka (QR Code) katika tili ya Lipa kwa Simu na niliweza kulipa moja kwa moja kutoka katika benki yangu.  Hii ina maanisha kwamba ninaweza sasa kufuatilia malipo yangu yote  kadri yatakavyokuwa yanafanyika kutoka benki,” aliongeza bi Mwajuma.

Send this to a friend