Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imesema Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwaka ulioishia mwezi Septemba 2022 umeongezeka hadi asilimia 4.8 kutoka asilimia 4.6 kwa mwaka ulioishia mwezi Agosti, 2022.
NBS imesema kuongezeka kwa mfumuko huo kumechangiwa na kuongezeka kwa mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula kwa kipindi cha mwaka ulioishia mwezi Septemba, 2022 ikilinganishwa na kipindi cha mwaka ulioishia mwezi Agosti 2022.
Baadhi ya bidhaa bei ni pamoja na
Mchele, Unga wa ngano, Unga wa mtama, Unga wa mahindi, Samaki wa maji baridi, Dagaa wakavu, Matunda, Karanga mbichi, Viazi mviringo, Maharage makavu ya kawaida, Maharage ya kombati, Soya, Njegere kavu na Kunde kavu.
Aidha, imesema mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwaka ulioishia mwezi Septemba, 2022 umeongezeka hadi asilimia 8.3 kutoka asilimia 7.8 kwa mwaka ulioishia mwezi Agosti, 2022.
Kwa upande mwingine, mfumuko wa bei ambao haujumuishi bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwezi Septemba, 2022 umeongezeka hadi asilimia 3.5 kutoka asilimia 3.4 kwa mwaka ulioishia mwezi Agosti, 2022.