Mgambo wadaiwa kuwakata mapanga wananchi

0
64

Madiwani wa Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga wamelalamikia vitendo vinavyofanywa na baadhi ya Mgambo wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wilayani humo wanaodaiwa kuwakata mapanga wananchi wanaowakamata wakiwa na mazao ya misitu.

Wakizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani cha halmashauri hiyo, Diwani wa Kata ya Iyenye, Lucas Makurumo amesema Aprili 6 mwaka huu mtu mmoja kwenye kata yake alijeruhiwa kwa kupigwa na kukatwa mapanga na mgambo hao nyakati za usiku, na mpaka sasa amelazwa hospitalini akiendelea na matibabu.

Aidha, madiwani wameongeza kuwa mgambo hao wamekuwa wakiwakamata wananchi wakiwa wamevaa soksi nyeusi ili kuficha sura zao wasitambulike, hali ambayo inaleta hofu kwa wananchi na inaweza kusababisha kuvunjika kwa hali ya usalama.

Hata hivyo Mkuu wa Jeshi la Polisi wilaya ya Kahama, Rockius Mulokozi, amethibitisha tukio la Aprili 6 na kusema kuwa alipigiwa simu na diwani hiyo kuhusu mgambo hao, na kwamba baada ya taarifa hiyo alituma askari kwenda kutuliza vurugu zilizokuwa zikiendelea.

Akijibu malalamiko hayo Meneja wa TFS, Ester Josephat amesema taarifa za wananchi kupigwa na mgambo wanazo na wameanza kufuatilia kwa ukaribu ili kuhakikisha kila anayehusika anachukuliwa hatua za kisheria, na kuongeza kwamba mgambo wao hawafanyi kazi kwa kuficha sura zao.

Send this to a friend