Kamati ya Ulinzi na Usalama imemkamata mganga wa kienyeji maarufu ‘Askofu’ katika Mhalo wa Mbamba Bay, Wilaya ya Nyasa kwa tuhuma za kuwauzia wavuvi wa Ziwa Nyasa dawa za miti shamba ambazo amedai zinasafisha nyota na kuzuia maambukizi ya UKIMWI iwapo watashiriki tendo la ndoa ziwani.
Mganga huyo ametiwa hatiani na Polisi walioambatana na Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Peres Magiri wakati mganga huyo akiendelea na shughuli zake za kuuza dawa hizo kwa wavuvi kwenye fukwe za Ziwa Nyasa.
“Wavuvi wanapaswa kuchukua tahadhari juu ya ugonjwa wa Ukimwi ambao unaambukizwa kwa kufanya ngono bila kinga. Hakuna mganga ambaye ana dawa za kutibu au kuzuia ugonjwa wa Ukimwi,” amesema Magiri.
Magiri amewataka wavuvi kuzingatia maadili na kufanya kazi zao kwa bidii pasipo kuruhusu ushawishi usiofaa kutoka kwa waganga ambao unaweza kuhatarisha maisha yao.