
Jeshi la Polisi mkoani Pwani linamshikilia kijana aitwaye Ally Juma Shaban (29) mganga wa tiba asilia na mkazi wa Makazi Mapya, Mlandizi kwa tuhuma za mauaji ya Juma Yoram Nyambihira (58) mkazi wa Makazi Mapya, Mlandizi.
Jeshi la Polisi limesema lilipokea taarifa kutoka kwa ndugu wa marehemu kupitia kituo cha Polisi Mlandizi wakieleza kupotea kwa ndugu yao tangu Agosti 17, mwaka huu, ambapo Jeshi la Polisi lilifungua jalada la uchunguzi na kuanza ufuatiliaji.
Baada ya uchunguzi lilimkamata mtuhumiwa huyo ambaye alikuwa akiishi na marehemu, ikielezwa kuwa ndiye aliyekuwa akimpatia matibabau ya tiba asilia nyumbani kwake kutokana na tatizo la uoni hafifu.
“Mnamo Septemba 3, 2025 Jeshi la Polisi likiendelea na upelelezi walifika nyumbani alipokuwa akiishi Juma na mtuhumiwa kwa ajili ya upekuzi wa kina ambapo walibaini kuwepo kwa tanuri la mkaa maeneo ya karibu na nyumba hiyo huku pembeni ya tanuri hilo kukiwa na dalili ya uwepo wa shimo,” imeeleza taarifa.
Imeongeza kuwa “Zilifanyika jitihada za kufukua shimo hilo na kukuta mwili wa marehemu. Mwili ulifanyiwa vipimo na daktari na kukabidhiwa kwa ndugu ili wafanye taratibu za mazishi. Mtuhumiwa wa kesi hii atafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.”
Aidha, Jeshi la Polisi limewahakikishia wananchi kuwa litaendelea kuimarisha usalama wa raia na mali zao kwa kuchukua hatua za kisheria kwa wote wanaoshiriki kufanya uhalifu wa aina yoyote.








