Mganga wa kienyeji akamatwa akiwa na fisi, adai anamtumia kusafiria

0
4

Jeshi la Polisi mkoani Simiyu limemkamata mtuhumiwa mmoja ambaye ni mganga wa kienyeji akiwa na fisi.

Taarifa ya Jeshi la Polisi imesema Januari 24, 2025, saa kumi na mbili jioni katika Kijiji cha Kilulu Kata ya Bunamala Tarafa ya Ntuzu wilayani Bariadi Jeshi la Polisi kupitia kikosi kazi cha kupambana na uhalifu, kilifanikiwa kumkamata Emmanuel John Maduhu (31), Msukuma na mganga wa kienyeji akiwa na mnyama huyo akiwa mzima.

“Mganga huyo alieleza kuwa anamtumia fisi huyo katika shughuli za uganga wa jadi ikiwa ni pamoja na kumtumia kama chombo cha usafiri anapotaka kupaa angani,” imeeleza.
Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Mamlaka za Wanyamapori wanaendelea na uchunguzi na mara baada ya upelelezi kukamilika, mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.

Aidha, Kamanda wa Polisi mkoani Simiyu ametoa wito kwa wananchi kuacha mara moja kufuga fisi kwani wanyama hao ni hatari hususan ni hivi karibuni ambapo kumekuwa na wimbi kubwa la watoto kuliwa na fisi.