Mgombea Urais Kenya aahidi mikopo kwa wanandoa wapya

0
41

Mtia nia wa kugombea urais nchini Kenya ameahidi kutoa mikopo yenye thamani ya kati ya TZS milioni 10 hadi TZS milioni 20 kwa wanandoa wapya endapo atachaguliwa katika ofisi hiyo ya juu zaidi nchini humo.

Gavana wa Machako, Alfred Mutua amesema hayo wakati akizindua ilani yake ya uchaguzi na kusema mikopo hiyo ya riba nafuu italipwa ndani ya miaka 20, na kwamba itawezesha wanandoa wapya kuanza maisha kwa wepesi.

Amesema lengo la mpango huo ni kuwezesha waliooana kuanza maisha kwa utu na kuboresha kiwango cha maisha yao ikiwemo kujenga nyumba za kisasa.

Aidha, amesema kuwa serikali yake itaelekeza kwamba upandaji miti uchukuliwe kama sehemu ya mahari. “Unapokwenda kulipa mahari, utatakiwa kusema na idadi ya miti uliyopanda.”

Wanasiasa nchini humo wameanza kampeni wakitafuta kuchaguliwa kumrithi Rais Uhuru Kenyatta ambaye ataondoka madarakani mwakani baada ya kumaliza muda wake wa miaka 10 madarakani.

Mwanasiasa nguli wa upinzani, Raila Odinga na Makamu wa Rais, William Ruto ndio wanaonekana ndio washindani wakuu zaidi kwenye uchaguzi huo wa Agosti 2022.

Hali ya uchumi, ajira kwa vijana na vita dhidi ya rushwa ni ajenda zinazozungumzwa zaidi na wanasiasa wanaoutafuta urais. Hata hivyo, chaguzi za nyuma zinaonesha kwamba Wakenya hupiga kura kufuata mrengo wa kabila kuliko sera za mgombea.

Send this to a friend