Mgombea wa upinzani Guinea ajitangaza kushinda Urais

0
35

Mgombea wa upinzani nchini Guinea, Cellou Dalein Diallo amejitangaza kuwa ameshinda uchaguzi mkuu wa Rais uliofanyika Jumapili.

Licha ya kuwa matokeo rasmi ya uchaguzi huo hayajatangazwa, Diallo amewaambiwa waandishi wa habari kuwa yeye ndiye mshindi, licha ya uchaguzi huko kugubikwa na kasoro mbalimbali.

Tume ya taifa ya uchaguzi imesema kuwa zoezi la uhesabuji kura linaendelea na kwamba wao ndio chombo chenye mamlaka ya kumtangaza mshindi.

Wafuasi wa mwanasiasa huyo walioingia mitaani kusherehekea ushindi huo walitawanywa na polisi. Kupitia ukurasa wa Twitter, Diallo amedai kuwa watu watatu wameuawa na wengine kadhaa wamejeruhiwa na maafisa wa polisi.

Matokeo ya uchaguzi huo wenye ushindani mkubwa yanatarajiwa kutangazwa Jumatano, ambapo wagombea watakuwa na siku nane kukata rufaa dhidi ya matokeo yatakayotangazwa.

Kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo, mgombea Urais anatakiwa kupata zaidi ya 50% ya kura zote halali ili atangazwe mshindi.

Endapo hakuna mgombea atakayefikisha idadi hiyo kutakuwa na duru ya pili ya uchaguzi itakayofanyika Novemba 24 mwaka huu.

Wananchi wa Guinea wameandamana kwa miezi kadhaa kupinga uamuzi aa Rais Alpha Condé kugombea nafasi hiyo kwa muhula wa tatu.

Send this to a friend