Mhadhiri asimamishwa kwa tuhuma za rushwa ya ngono

0
40

Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) kimemsimamisha kazi Mhadhiri, Adam Semlambo ili kupisha uchunguzi kuhusu tuhuma ya rushwa ya ngono baada ya kusambaa kwa video iliyomuonesha akifanya ngono, kinyume na maadili ya utumishi wa umma.

Kaimu Mkuu wa chuo hicho, Dkt. Cairo Mwaitete amesema kuwa, uongozi wa chuo hicho umelazimika  kumsimamisha kazi kwa muda kuanzia Machi 2 mwaka huu ili kupisha uchunguzi wa tuhuma hizo.

“Baada ya kuipata video hiyo chafu ikimuonesha mhadhiri wetu akiwa mtupu na mwanamke jana majira ya saa 12 jioni, tulimuita ofisini na kumhoji na alikiri kuhusika ila alidai ni mambo yake ya mtaani, hivyo sisi kama uongozi tumeamua kumsimamisha kazi kupisha uchunguzi,” amesema Kaimu

Aidha Dkt. Mwaitete amesisitiza kuwa chuo kimesikitishwa na tukio hilo, na kamwe hawatolifumbia macho suala hilo kwa kuwa linachafua taswira ya chuo chao, hivyo wamefanya hivyo ili kulinda sifa ya chuo, na wazazi waendelee kuwaamini.

Pia ameongeza kuwa, kwa sasa hawajajua kama mwanamke aliyekuwa akifanya naye ngono ni mwanafunzi wa chuo hicho au la maana picha haimuonyeshi vizuri na ndio maana wameamua kuiachia vyombo vya usalama.

Uongozi wa chuo hicho umelaani vitendo hivyo na tayari umetoa taarifa kwa umma kuelezea hatua zilizochukuliwa kufuatia mhadhiri huyo kudaiwa kuhusika na vitendo vya rushwa ya ngono kwa wanafunzi wake.

Send this to a friend