Mhitimu kidato cha Nne afariki kwa mpenzi wake akisherehekea siku yake ya kuzaliwa

0
7

Msichana mwenye umri wa miaka 19, aliyemaliza masomo yake ya Kidato cha Nne hivi karibuni, amefariki dunia kwa mazingira ya kutatanisha akiwa nyumbani kwa mpenzi wake katika eneo la Lang’ata, Nairobi, wakati wa kusherehekea siku yake ya kuzaliwa.

Binti huyo, Faith Momanyi, aliyetarajiwa kujiunga na chuo kikuu mwaka huu, aliondoka nyumbani kwa wazazi wake ili kusherehekea siku yake ya kuzaliwa pamoja na marafiki zake. Kundi hilo la watu watano lilianza sherehe zao katika klabu maarufu kando ya Barabara ya Lang’ata, wakifurahia usiku wa burudani.

Baada ya muda, marafiki walitawanyika, na Faith akaelekea nyumbani kwa mpenzi wake pamoja na rafiki yake wa kike. Hata hivyo, muda mfupi baada ya saa sita usiku, rafiki yake aliondoka na kumwacha Faith peke yake na mpenzi wake.

Siku iliyofuata, rafiki yake aliposhindwa kumpata Faith kwa simu, alianza kuwa na wasiwasi, na ilipofika saa kumi na moja jioni, alipokea simu kutoka kwa mpenzi wa Faith akimwarifu kwamba rafiki yake alikuwa amefariki dunia.

Mmoja wa mashahidi ameeleza “yeye alienda kazini akarudi saa 11 jioni, nikakutana naye kwa ngazi, akaniuliza kama niko na funguo, nyumba ilikuwa imefungwa. Ghafla akapata funguo ya akiba na akaifungua. Alipofungua akaniita akisema Faith yuko kitandani amekufa. Nilienda nikamshika, alikuwa amefariki.”

Uchunguzi wa mwili wake ulithibitisha kuwa Faith alifariki kutokana na ukosefu wa hewa, huku kiasi kikubwa cha maji kikikutwa kwenye mapafu yake. Uchunguzi unaendelea huku wakiendelea kumshikilia mpenzi wa Faith.